January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Pigo la pili Dk. Mahanga, Mtaa wa Migombani waapishana

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Migombani, Japhet Kembo (kushoto) akimsikiliza Mwanasheria Idd Msanga.

Spread the love

ILE sinema ya kuvutia iliyomfikisha kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa jimbo la Segerea, Dk Makongoro Mahanga, kunusurika na kipigo cha “umma” kwa kuokolewa na Polisi, haijafika tamati, anaandika Pendo Omary.

Iliendelea Jumatatu hii baada ya sehemu yake ya kwanza kutimia tarehe 7 Desemba, pale wananchi wema wa Mtaa wa Migombani, Segerea, Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam, kufanikiwa kumzuia kiongozi wasiyemchagua kuapishwa kwenye ukumbi wa manispaa wa Anatouglo, Mnazimmoja.

Hali ya mambo ilionesha Dk. Mahanga alitia uzito mpango mchafu wa chama cha CCM uliolenga kushinikiza utaratibu umtambue na kumuapisha mgombea wao hasa kwa kuwa ndiye alipewa barua rasmi ya kuitwa kwenye hafla hiyo ya uapishaji viongozi wapya.

Mwandishi wa MwanaHALISIOnline alishuhudia tukio hilo la kihistoria la wananchi hao waliojaa furaha, kusimamia uapishaji wa kiongozi waliyempa ridhaa, Japhet Albert Kembo, badala ya Uyeka Iddi Lumbyambya, ambaye alilazimishwa kuwa mshindi na mfumo wa kidhalimu.

Kembo, alichaguliwa kwa kura 547, akiwa amewashinda wagombea wawili akiwemo Uyeka wa CCM aliyepata kura 273.

Mgombea mwingine alikuwa Mchatta Erick Mchatta, wa Chama cha NCCR-Mageuzi, ambaye alipata kura 205. Kura zote zilizopigwa zilikuwa 1,024. Mbili ziliharibika.

Uapishaji huo ulitekelezwa kwa usimamizi wa Wakili wa Kujitegemea jijini, Idi Msawanga, mbele ya halaiki ya wananchi wakazi wa Mtaa wa Migombani huku zikiamka shangwe na vigeregere vilivyohanikiza ilipo ofisi ya serikali ya mtaa huo.

Genge la wana-CCM lilitaka kuhakikisha kuwa Kembo, aliyewakilisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na kushinda uchaguzi huo wa 14 Desemba, anapigwa pande asitambuliwe, na asiongoze.

Ushahidi kwamba Kembo alichaguliwa kihalali unaonekana kwenye fomu ya matokeo ambayo Msimamizi wa uchaguzi, Shamsu Ramadhani Sasiro, ameweka saini yake kwenye Fomu ya Uchaguzi Na. V, akiidhinisha kuyatambua matokeo.

Msimamizi huyo pia amegonga muhuri kwenye fomu hiyo ambayo kwa sababu anazozijua binafsi, Uyeka hakusaini katika sehemu yake. Mchatta  yeye alisaini pake.

Taarifa zilizopatikana zimesema Kembo alinyimwa barua rasmi ya kuitwa kuhudhuria hafla ya uapishaji viongozi wapya, ikiwa ni njama ya makusudi iliyolenga kumpenyeza Uyeka achukue nafasi asiyostahiki.

Wakati tukio la kuapisha likitekelezwa na Wakili Msawanga, ofisi ya mtaa ilikuwa imefungwa na Afisa Mtendaji wa Mtaa, Suzan Zephania, hakuwepo maeneo hayo. Baadaye alijitokeza.

Wakili Msawanga, mara baada ya kutekeleza uapishaji uliohusisha pia wajumbe wa serikali ya mtaa huo, alisema, “Leo nimewaapisha viongozi wa serikali ya mtaa akiwemo mwenyekiti, wajumbe watatu wa kamati ya mtaa waliohudhuria, huku wajumbe wengine wakiomba udhuru.

“Nimeifanya kazi hii baada ya kuombwa na wananchi wa Mtaa wa Migombani hapa jimboni Segerea, ikiwa ni sehemu muhimu ya kutimiza majukumu kwa mujibu wa sheria,” alisema huku akishangiliwa na wananchi.

Wajumbe walioapishwa pamoja na Mwenyekiti Kembo, ni Nyangeta Flora Justine, Rose Benard, Ramadhani Rashid Seif. Waliopata udhuru ambao wataapishwa wakati mwingine ni Paulina Mbalale na Anjelo Machunda.

Kembo alisema kilichofanyika ni kielelezo cha namna utawala mbaya unavyowafikisha wananchi kuamua kusimamia sheria.

“Wananchi wamechoka kukaa bila ya huduma za serikali ya mtaa wao. Leo saa 2:30 asubuhi wamekuja nyumbani kwangu na kunitaka niende ofisi ya serikali ya mtaa nikaapishwe. Sikuwa na jinsi zaidi ya kuwasikiliza na kuheshimu matakwa yao ambayo naona ni halali maana walituchagua katika uchaguzi halali.”

Mtendaji Suzan alipozungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema alikosa kuwepo mapema ofisini kwa sababu hakuwa na taarifa za tukio hilo.

“Siwezi nikafanya naye kazi hadi nipate barua ya uthibitisho wa kuapishwa kwake kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Segerea,” alisema alipoulizwa kama anatambua uongozi mpya. Haikuwezekana kumpata afisa mtendaji huyo, Justine Nyangwe.

Baadhi ya wananchi walisikika wakisema, “tumechoka kwa kweli. Tumebadilisha uongozi baada ya kuchoshwa na uongozi usioheshimu wananchi, hawasikilizi kero zetu na kuzitafutia ufumbuzi.”

Obedi John yeye alisema sasa wana imani kuwa viongozi wapya watawasikiliza wananchi na kushirikiana nao katika kuondoa kero mbalimbali.

“Angalia vituko vya serikali ya CCM, tumechagua viongozi tunaowataka, lakini tayari zimepita siku 30 bila ya kuwaapisha. Sababu ni kutaka kutuwekea kiongozi wanayemtaka wao. Hapo hatukubaliani, si halali,” alisema mama aliyekataa kujitambulisha.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala, Issaya Mungurumi, alipoulizwa sababu za kutowaapisha viongozi waliochaguliwa na wananchi kwa mujibu wa sheria, alisema atakuwa tayari kueleza kwa undani iwapo atafuatwa ofisini siku nyingine.

Alipoelezwa kwamba wananchi wameshaapisha viongozi wao chini ya usimamizi wa wakili wa kujitegemea, alisema, “sina taarifa za hilo unalonieleza. Sijui kama wameapishwa.”

Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Samwel Binagi alisema kama wananchi wameamua kuchukua hatua ya kuapisha viongozi wao inavyotakiwa, haoni tatizo la kisheria.

“Mimi sina tatizo na uamuzi waliouchukuwa wa kuwaapisha viongozi waliowachagua. Kwa kweli ni haki yao,” alisema kwa msisitizo huku akiwa amezungukwa na wananchi.

error: Content is protected !!