LICHA ya kuitwa mtu wa hovyo, mchekeshaji anayechipuka kwa kasi Peter Mollel ‘Pierre’ sasa ni lulu. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Kuitikia kwake mwaliko aliopewa wa kuwa mgeni maalum wa Mariamu Ditopile, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) bungeni jijini Dodoma leo tarehe 3 Aprili 2019, kumeenda sambamba na ‘kulamba dume’ kutoka kwa Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa.
Pierre alikutana na Waziri Majaliwa ambaye alionesha kufurahishwa kwake kwa kukutana na mchekeshaji huyo.
Baada ya kupiga picha na Waziri Majaliwa, amemuahidi kumpa tiketi ya ndege kwa ajili ya kwenda kuishangilia Stars katika michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Misri.
Wakati wa kutambulishwa kwake, Pierre ameshangiliwa na baadhi ya wabunge kuonesha umuhimu wake. Nderemo hizo zimefanyika licha ya kuitwa mtu wa hovyo wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Kuchangia Ujenzo wa Shule ya Wasichana Kisarawe, Pwani uliopewa jina la ‘Tokomeza Ziro’ mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Spika Job Ndugai alimpa nafasi maalum Ditopile amtambulishe Pierre kwa kuwa yeye hamfahamu.
“Nina mgeni lakini simfahamu, naomba nimpe heshima Mheshimiwa Mariamu Ditopile atumie dakika moja kumtambulisha maana simfahamu,”amesema Spika Job Ndugai.
Akimtambulisha Pierre, Ditopile alisema ni Mtanzania (huku akisimama na kujipinda) mzalendo mjasiriamali wa fenicha anaepatikana Changombe. Ni mpenda burudani na ana kijiwe kinachoitwa Liquid.
“Lakini hivi karibuni ametokea kupata umaarufu wa hali ya juu, sio kwa nchi yetu hadi nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na sanaa na vichekesho.
“Ndugu Pierre ni maarufu na kwa kauli zake ambazo huwafurahisha watu na hata kama una msongo wa mawazo, anauondoa.” amesema.
Hata hivyo, mbunge huyo ameeleza mchango wa Pierre katika kuleta hamasa kwa timu ya Taifa – Taifa Stars – kushinda bao 3 -0 dhidi ya Uganda.
“Ndugu Pierre karibu sana bungeni,” amesema Ndugai na kuongeza “Magufuli utabaki kuwa juu utabaki kileleni.”
Pia Pierre ameonekana kukonga nyoyo za baadhi ya wabunge ambapo baadhi yao pamoja na wafanyakazi wa Bunge kwa wakati tofauti, walipiga picha naye.
Leave a comment