January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Picha za mauaji Kenya zaumiza wahariri

Rais Mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki

Spread the love

USIOMBE kuona picha za mwenendo wa matukio ya ghasia yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya wa Disemba 2007. Zinaumiza kuliko kawaida, kuliko mtu unavyoweza kufikiria. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea) .

Na maumivu makubwa waliyoyapata baada ya kuziona, ndiyo yaliwasukuma wahariri wa vyombo mbalimbali vya Tanzania kutambua kuwa wakitaka wataiepusha nchi yao na balaa lililoikumba Kenya baada ya uchaguzi. 

Mwaka huu, ni mwaka wa uchaguzi mkuu Tanzania ambapo Oktoba 25 ndiyo siku ya kupiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani. Wazanzibari watakuwa na kura ya rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani.

Ilikuwa ni kipindi cha mada ya utendaji bora katika mafunzo ya kuwapiga msasa wahariri wa Tanzania yaliyoandaliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), mjini Morogoro, mwandishi na mtangazaji Joseph Warungu aliwashitua wahariri kwa kuwaonesha picha hizo.

Video ya muda usiozidi dakika kumi ilionesha picha za harakati za Wakenya kuuana wenyewe kwa wenyewe, kujeruhiana kwa silaha za moto na za jadi; maelfu wakauliwa, wengine wengi zaidi wakakimbia makazi yao na kujikuta wakihifadhiwa kwenye kambi za ukimbizi ndani ya nchi yao.

Warungu, raia wa Kenya aliyefanya kazi kwa zaidi ya miaka 15 na BBC, akiwa Idhaa ya Kiswahili, lakini akitangazia pia vipindi vya Kiingereza kuhusu masuala ya barani Afrika, alisema waandishi wa Kenya walijisahau wakidhani kila walichokuwa wakifanya ni sahihi. 

“Waandishi tuliamini tupo sahihi, kumbe imetokea tumechangia machafuko yaliyotokea. Tuligutuka dakika za mwisho hali ikiwa mbaya na tayari mamia ya Wakenya wenzetu wamepoteza maisha. Tuliacha kutenda kazi kwa uadilifu tukaangalia maslahi mengine,” alisema huku akiwageukia wahariri wapatao 40 kwa kuwasihi wachukue hatua ili kunusuru Tanzania isije kuifuata Kenya.

Warungu alisema katika wakati kama huu Tanzania inapokabiliwa na uchaguzi mkuu, wahariri wana jukumu zito ambalo lazima walitekeleze kwa uadilifu na kwa kufuata maadili ya kitaaluma ya uandishi wa habari.

Alisema uandishi wa kufikiria makabila na ushabiki wa kisiasa, utachochea chuki na kujenga uwezekano wa kusababisha machafuko. Kwamba, wanasiasa wana hatari wasipoangaliwa kwa makini. 

“Tusiwafuate kwa kila wanalolitaka tulifanye. Tutumie akili zetu na tuzitumie akili katika namna ya kujali na kulinda maslahi ya nchi na wananchi, sio wanasiasa wabaya,” alisema. 

Alisema wahariri nchini Kenya walishtuka wakati tayari maelfu ya raia wamekufa, wakati walikuwa na muda wa kutafakari na kuchukua hatua ifaayo na kuepusha janga.

“Niwaambie tunao mchango muhimu na tuoneshe dhamira kwa faida ya nchi. Sisi waandishi Kenya tulikosea, wenzetu mjifunze kwa kuwa waangalifu kwa mnavyofanya kazi ili kuinusuru nchi na balaa,” alisema. 

Kenya iliingia katika machafuko baada ya utawala wa Rais Mwai Kibaki, kuvuruga matokeo ili kulazimisha ushindi dhidi ya kundi la ODM chini ya Raila Odinga. Baada ya Tume ya Uchaguzi chini ya Samuel Kivuitu, kumtangaza Kibaki mshindi, kulifumuka maandamano yakaenea nchi nzima.

Wahariri walipogutuka, walikutana na kujadiliana na kutoa tamko la kutaka Wakenya waache chuki ili kunusuru nchi yao ya kusambaratika zaidi. Vyombo vyote vilichapisha na kutangaza tahariri ukurasa wa mbele.

error: Content is protected !!