Spread the love

 

MCHANGO wake Naibu Rais wa Kenya, William Ruto wa Sh milioni 20.3 kwa kukindi akiba na mikopo kilichoundwa na wanawake wanaojihusisha na biashara haramu ya ukahaba nchini humo ‘madada poa’ umezua zigo baina ya makundi mawili ya wanawake hao. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Ruto ambaye pia ni mgombea urais nchini humo katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka kesho, aliwachangia fedha hizo wanawake hao kwa lengo la kuwasaidia kuunda kikundi cha kuwekeza kwenye miradi mbalimbali na kujikomboa kutoka kwenye biashara hiyo haramu.

Ruto aliahidi kuwasaidia akina dada hao wa mji wa Mtito Andei, kaunti ya Makueni nchini humo, akilenga kuwaonesha juhudi zake za kuhuisha uchumi watu wa kipato cha chini.

“Undeni chama cha akiba na mikopo na mtafute mbinu mbadala za heshima za kujipatia riziki,” Ruto aliwaambia wanawake hao ambao walipata nafasi ya kuzungumza naye alipotembelea eneo hilo miezi miwili iliyopita na kufanya mkutano wa kampeni.

Aidha, kiongozi huyo alitimiza ahadi yake wiki iliyopita na pesa hizo zikazua vita kati ya wanawake hao.

Zogo hilo liliongezeka wiki hii baada ya kuibuka kuwa kundi moja lililokuwa limetumia nusu ya pesa hizo bila kuhusisha wenzao.

Madada poa hao 46 walimlaumu Caroline Mumbua, mwanamke aliyezungumza kwa niaba ya wenzake katika mkutano wa Ruto, kwa kutumia visivyo pesa hizo.

Hata hivyo, kundi linaloongozwa na Mumbua lililaumu kundi linalolalamika kwa kumezea mate pesa hizo.

“Naibu Rais alitoa pesa hizo kupiga jeki uchumi wa makahaba wote wa Mtito Andei, lakini Carol anagawia marafiki na jamaa zake na kutumia zinazobaki kwa miradi anayotaka bila idhini yetu,” alidai Faith Mwikali.

Mumbua alisisitiza kuwa ingawa pesa hizo zilinuiwa kufaidisha makahaba wote wa mji wa Mtito Andei, wanatakiwa kujiunga na chama hicho cha ushirika.

“Muda wa usajili umepita. Hatutambui yeyote asiye mwanachama wa chama hiki,” Mumbua aliambia gazeti moja nchini humo.

Alikiri kwamba, ametumia nusu ya pesa hizo kugawia wenzake, kununua hema, viti na vyombo vya muziki vya kukodisha na kundi lake lakini akakanusha kuwa aliondoa baadhi ya maofisa wa kundi na kujaza nafasi zao na jamaa zake.

Imeelezwa kuwa baadhi ya maofisa wa usalama katika eneo hilo ni miongoni mwa walionufaika na ukarimu wa Mumbua.

Mwanamume aliyesaidia kundi hilo kuandika maazimio ya mkutano wa kundi hilo alikiri kwamba alilipwa Sh400,000.

Bi Mumbua alisema Sh milioni 10 zilizobaki zitatumiwa kwenye mpango utakaofaidisha wanachama 38 waliosajiliwa katika chama hicho.

Mwikali amesisitiza kuwa baada ya kupata pesa kutoka kwa Ruto, Mumbua aliwatema baadhi ya makahaba wenzake.

“Baada ya pesa kuingia katika akaunti, Carol alitutenga. Anatufukuza tunapoenda kuchukua kondomu zilizotolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali kama tulivyokuwa tukifanya kila siku lakini cha ajabu siku hizi anatufukuza, sio kama zamani,” aliongeza Mwikali.

Kundi la Mumbua linasema wanaolalamika wanachochewa na wanasiasa wa eneo hilo waliomlaumu Ruto kwa kuahidi kuwasaidia.

Wakati Mwikali na kundi lake wamesema pesa hizo zimewaongezea maswahibu kwani wateja wao wamekuwa wakikataa kuwalipa wakidai naibu rais aliwapa pesa kwa niaba yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *