KIUNGO Mshambuliaji wa klabu ya Juventus ya Italia, Paul Pogba huenda akakumbana na adhabu ya kufungiwa hadi miaka minne kujihusisha na masuala ya soka baada ya kupatikana na kosa la matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini. Anaripoti Isaya Temu, TUDARCo…(endelea).
Uchunguzi huo ulifanyika baada ya mechi ya Juventus dhidi ya Udinese iliyofanyika tarehe 20 Agosti 2023 ambapo Pogba aligundulika kutumia dawa za kusisimua misuli, kuongeza nguvu kosa ambalo adhabu yake hufikia hadi miaka minne.
Kwa mujibu wa Mahakama ya Italia ya kupambana na dawa za misuli (NADO) iliyotolewa leo tarehe 12 September 2023, imesema kuwa imemfungia kwa muda Pogba wakati akisubiri majibu ya kipimo cha sampuli “B” ya kielelezo alichochukuliwa.
“Kwa kukubali maoni yaliyopendekezwa na Mwendesha Mashtaka wa Taifa wa Kupambana na Dawa za Kulevya, NADO imemsimamisha kwa muda mwanasoka Pogba,” imeeleza taarifa ya NADO Italia.
Wakala wake Rafaela Pimenta amesema kuwa wanasubiri kukamilika kwa taarifa ya uchunguzi na kwa sasa hawawezi kusema chochote.
“Jambo la uhakika ni kuwa Pogba hakutaka kuvunja sheria na huenda akawa hana hatia” amesisitiza Rafaela.
Klabu ya Soka ya Juventus imesema kwamba imepokea amri ya NADO na wao kama kampuni watatathmini hatua zao kuelekea jambo hilo.
“Leo mchezaji Paul Labile Pogba amepokea amri ya kusimamishwa kwa muda kutoka Mahakama ya Kitaifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya kufuatia matokeo mabaya ya uchambuzi uliofanywa 20 Agosti 2023. Kampuni ina haki ya kutathmini hatua zijazo za kiutaratibu,” imeeleza taarifa ya Juventus.
Tangu ahamie Juventus kutoka timu ya mashetani wekundu Manchester United msimu uliopita, Pogba amecheza jumla ya dakika 162 bila kufunga goli kutokana kuwa na majeruhi ya mara kwa mara.
Leave a comment