Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari Paul Makonda kizimbani kesho
Habari

Paul Makonda kizimbani kesho

Paul Makonda
Spread the love

 

ALIYEKUWA Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Christian Makonda, kesho Alhamisi, tarehe 3 Februari 2022, atapanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni jijini Dar es Salaam kujibu mashitaka ya jinai yanayomkabili. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Ni katika kesi ya jinai iliyosajiliwa mahakamani kama Miscellaneous Criminal Application Na. 1 ya mwaka 2022, itakayosikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Aron Lyamuya.

Kesi hiyo imefunguliwa na Mwandishi wa Habari mwandamizi, Saed Kubenea ambaye anawakilishwa jopo la mawakili wakiongozwa na Nyaronyo Mwita Kicheere na Hekima Mwasipu.

Kubenea aliyewahi kuwa mbunge wa Ubungo, Dar es Salaam kati ya 2015-2020 anamtuhumu Makonda kwa makosa mbalimbali.

Miongoni mwa makosa hayo, ni matumizi mabaya ya madaraka ya umma, wakati akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Makonda anadaiwa kuwa siku ya tarehe 17 Machi 2017, akiwa na watu waliobeba silaha za moto, alivamia Clouds TV na kumuagiza mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu kurusha video inayomwonesha mwanamke aliyejulikana kwa jina la Grace Athuman.

Katika video hiyo, ambayo haijulikani nani ameiandaa, mwanamke huyo alidaiwa kuonekana akifanya tendo la ndoa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Kwa mujibu wa ushahidi wa video za CCTV, Makonda anaonekana kuvamia kituo cha Clouds saa nne usiku, akiwa anaendesha mwenyewe gari namba T553BFM.

Vilevile, Camera za CCTV pamoja na kitabu cha kumbukumbu za walinzi, vinamuonesha Makonda aliingia Clouds akiwa na askari wanne waliokuwa na sare tofauti za majeshi ya ulinzi na usalama, kati yao watatu wakiwa na silaha za moto.

Askari hao waliingia hadi chumba cha utangazaji, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za utangazaji, huku Makonda akitumia vitisho dhidi ya wafanyakazi wa Clouds kwa kutumia silaha za moto.

Kwa mujibu wa hati ya kiapo ya Kubenea, kitendo cha Makonda cha kuvamia televisheni ya Clouds, tena akiwa ameongozana na askari waliobeba silaha za moto, ni kinyume cha sheria ya Kieletroniki na Posta ya mwaka 2010.

Maombi ya kutaka kumshitaki Makonda yamewasilishwa mahakamani, chini ya kifungu cha 99 (1) cha Sheria ya mwenendo wa mashauri ya Jinai, Sura ya 20.

Kubenea anasema, hatua ya Makonda kuvamia Clouds, ni matumizi mabaya ya madaraka, chini ya kifungu cha 96 ya Kanuni ya adhabu (Penal Code), Sura ya 20 na kuingilia moja kwa moja, mawasiliano ya Kieletroniki.

Mbali na Makonda, wengine walioitwa mahakamani siku hiyo, ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Wawili hawa wanadaiwa wameshindwa kuchukua za kumfungulia mashitaka ya jinai mtuhumiwa huyo.

Maombi ya kumshitaki Makonda yameambatanishwa na wito maalum (Chamber Summons) na hati ya kiapo (Charge Sheet).

Katika kujenga hoja yake mahakamani, wakili wa Kubenea ameambatanisha ripoti ya uchunguzi ya Kamati Maalum iliyoundwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.

Ripoti ya Nape iliyochunguza tukio la kuvamiwa Clouds, ilimtia hatiani Makonda na kupendekeza kwa mamlaka yake ya uteuzi, kumchukulia hatua za kinidhamu; Makonda mwenyewe kuwajibika binafsi na kuwaomba radhi Clouds na wananchi kwa ujumla.

Hata hivyo, mapendekezo yote ya Kamati ya Serikali hayakutekelezwa. Muda mfupi baada ya Nape kumaliza kusoma ripoti yake kwa waandishi wa habari, Rais John Magufuli alitangaza kumfuta kazi.

Nape alirejea kwenye baraza la mawaziri hivi karibuni, kufuatia Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alishika madaraka ya urais baada ya kifo cha Magufuli, kuamua kumrejesha katika wizara hiyo.

Kamati ya Nape ilithibitisha kuwa Makonda alivamia kituo hicho cha televisheni akiwa anaendesha mwenyewe gari lenye namba T553 BFM na kuingia hadi chumba cha utangaji, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za utangazaji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

HabariSiasa

Dk. Rose Rwakatare atoa kadi 500 kila Wilaya Morogoro

Spread the loveMWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk...

ElimuHabari

CBE, WMA wasaini makubaliano wanafunzi kusoma wakifanyakazi

Spread the loveNAIBU Spika Musa Azzan Zungu amekipongeza Chuo cha Elimu ya...

HabariTangulizi

Dk. Slaa, Mwabukusi kuhojiwa na jeshi la Polisi Mbeya

Spread the loveJESHI la Polisi jijini Mbeya, linawashikilia kwa mahojiano Dk. Wilbroad...

HabariHabari Mchanganyiko

Kairuki Hospital Green IVF  yawanoa madaktari kuhusu upandikizaji mimba

Spread the love KITUO cha Upandikizaji Mimba cha Kairuki Hospital Green IVF...

error: Content is protected !!