June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Patricia apania nidhamu kwenye taarabu

Spread the love

PATRICIA Hillary ambaye ni mwanamuziki mkongwe wa Taarabu Asili nchini ameweka dhamira ya kurejesha hadhi ya muziki huo, anaandika Regina Mkonde.

“Napanga namna ya kurejesha hamasa ya kuandika na kuimba nyimbo zinazojenga maadili na si kubomoa wala mipasho kama ilivyo sasa. Uamuzi huu unaweza kuhamasisha wanamuziki wa namna hii kubadilika,” amesema.

Akizungumza na MwanaHalisi Online leo jijini Dar es Salaam, Patricia ameonesha kusikitishwa na mwenendo wa taarabu za kisasa zinavyoimbwa na kuchezwa na kwamba, bendi nyingi za muziki huo zipo kibiashara zaidi na kuacha maadili ya taarabu.

“Muziki wa kisasa wa taarabu si mbaya, ila uko kibiashara zaidi, kitendo kinachoshusha na kupoteza muelekeo wa muziki huu nchini, enzi zetu tulifanya taarabu zenye maadili na ujumbe ila za sasa zimelenga mipasho,” amesema Patricia.

Patricia amesema, uvaaji na uchezaji wa kisasa unaofanywa na baadhi ya bendi za taarabu hauendani na maadili ya nchi hii na kwamba unapotosha uhalisia wa muziki huo.

Hivi karibuni Patricia anatarajia kutoa nyimbo mbili mpya zitakazotambulika kama ‘Ngoma Zetu’ na ‘Ni Sisi’.

“Nataka niimbe nyimbo zenye ladha tofauti tofauti kama taarabu, mduara, jazband na vigodoro. Nia yangu ni kuondoa ukimya na kuwapa mashabiki wangu burudani ya nguvu,” amesema na kuongeza;

“Nataka kukumbushia enzi ya kale siku zote hayapotei, hayaishi ladha wala hayachoshi, siyo kama sasa taarabu inatolewa Januari, Septemba inachuja.”

error: Content is protected !!