Wednesday , 24 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Panya kuokoa waliofukiwa na kifusi
Habari Mchanganyiko

Panya kuokoa waliofukiwa na kifusi

Spread the love

 

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kimeanza kufundisha panya namna ya kutambua watu waliofukiwa na kifusi cha majengo, machimbo ya migodi na majanga mengine. Anaripoti Seleman Msuya…(endelea).

Teknolojia hiyo ya kumwezesha panya kubaini watu waliofukiwa ni mwendelezo wa chuo hicho, kutumia mnyama huyo kutambua vitu hatari kwa binadamu.

Hadi sasa panya wa SUA wamegundua mabomu katika nchi za Msumbiji, Angola na Cambodia, huku nchini wakiwa wanatumika kutambua ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB).

Akizungumza na mwandishi wa habari hii juzi kwenye Maonesho ya 17 ya Vyuo Vikuu nchini katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Naibu Mkuu wa SUA, Taaluma,

Profesa Maulid Mwatawala amesema chuo kupitia walimu wake, kimefanya utafiti wa kutatua changamoto kwa jamii ukiwamo wa panya kugundua mabomu, TB na sasa watu waliofukiwa na kifusi.

Profesa Mwatawala amesema kupitia panya waliogundua mabomu akiwemo Magawa na wanaotambua TB, chuo hicho kimetambulika kimataifa na kuwa chuo namba moja nchini kwa utafiti.

“Sisi ni chuo cha kwanza kwa utafiti nchini, lakini pia mtafiti bora nchini anatoka Sokoine, ila zuri zaidi kati ya watafiti 50 bora nchini zaidi ya 20 wanatoka hapa,” amesema.

Amesema baada ya mafanikio hayo, kwa sasa wanaendelea kutoa mafunzo kwa panya ili waweze kutambua watu wakifukiwa na kifusi, hali ambayo itawezesha kuokoa watakaokuwa hai.

“Mafanikio ambayo yameonekana kutambua mabomu na TB ni makubwa sana kwetu SUA. Ila kwa sasa tunawaandaa panya wetu watambue watu wanapofukiwa kwenye majengo, machimbo mbalimbali,” amesema.

Amesema baada ya mafunzo hayo kukamilika, panya ataokoa watu kwa kuingia kwenye kifusi akiwa na kamera maalumu, itakayompa taarifa mwokoaji ajue aliko mtu wanayehitaji kumwokoa.

“Tumeamua kumtumia panya kuokoa mtu kwenye kifusi kwa sababu hayo ndiyo mazingira yake, tofauti na kutumia mbwa au mnyama mwingine,” amesema.

Amesema panya ni mnyama wenye uwezo mkubwa wa kunusa, hivyo imani yao baada ya mafunzo hayo, wataendelea kusaidia jamii.
“Panya wa kuokoa mtu kwenye kifusi tutamekea kamera itakayorusha mawasiliano nje, hivyo kurahisishia kazi waokoaji,” amesema.

Profesa Mwatawala amesema mchakato wa kumfanya panya atofautishe binadamu na vitu vingine kwenye kifusi, unahitaji muda na si jambo la ghafla.

Amesema matokeo chanya ya panya, yameonekana kimataifa zaidi ambapo Msumbiji jimbo la Manica ni salama sasa baada ya panya kutegua mabomu.

“Angola na Cambodia, panya hasa Magawa, alifanya mambo makubwa katika historia ya wanyama, kwani alikuwa mnyama aliyetambua mabomu mengi na kutunukiwa medali ya dhahabu,” amesema.

Katika kutambua sampuli za kifua kikuu, panya wa SUA wamesaidia sekta ya afya kupambana na ugonjwa huo.

“Katika utambuzi, panya wetu wanaweza kutambua ugonjwa kwa dakika mbili, tofauti na maabara, hali hiyo inasaidia mtaalamu wa maabara kuchunguza sampuli zilizotambulika,” amesema.

Aidha, Naibu Mkuu wa Chuo amesema panya hao wamekiwezesha chuo kupata fedha za miradi, na hivyo kutekeleza malengo yake makuu yakiwamo ya utafiti na mafunzo.
“Dunia inaitambua SUA kutokana na utafiti wetu, ukiwamo wa panya watambuzi na hii imetafsiri sifa ya chuo kikuu. Sifa ya chuo kikuu ni utafiti na si wingi wa majengo,” amesema.

Profesa Mwatawala amesema panya wanaotumiwa na watafiti chuoni hapo ni wale wakubwa wa porini, wajulikanao kama panya buku.

Kwa upande mwingine Profesa Mwatawala amesema chuo kinaendelea na utafiti utakaowezesha matumizi ya bundi kutambua panya waharibifu mashambani na kuwaangamiza.

“Utafiti unaendelea, kufundisha, kutunza na kuzalisha bundi wa kukabiliana na panya waharibifu mashambani,” amesema.
Amesema kuna tafsiri mbalimbali kuhusu bundi, ila kwa mujibu wa utafiti wao, wanamwona ndege huyo kuwa ataokoa mkulima dhidi ya madhara ya panya.

Profesa amesema mikakati yao ni kufanya utafiti utakaochochea maendeleo, uchumi na huduma za jamii.

Amesema wanaandaa wanafunzi ambao wakimaliza masomo wajiajiri.

Ameongeza kuwa SUA itatekeleza malengo ya Serikali kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na mkombozi wa nchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Bodaboda waeleza mafanikio mafunzo usalama barabarani

Spread the loveMADEREVA bodaboda katika Jiji la Dodoma wameeleza jinsi mafunzo ya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yaahidi kuendelea kuunga mkono Serikali za Mitaa

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya...

Habari Mchanganyiko

Watuhumiwa 12 wa kilo 726.2 za dawa za kulevya wafikishwa mahakamani

Spread the love  WATUHUMIWA watatu wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Mkoani...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!