July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Panya kalowa’ watinga bungeni

Spread the love

 

BAADA ya kikundi cha vijana wahalifu katika jiji la Dar es Salaam kutikisa kwa jina la ‘Panya Road’, Mbunge wa Viti Maalum, Fatuma Toufiq (CCM) ameibuka na kudai kikundi kingine cha uhalifu maarufu kama ‘Panya Kalowa’ kimeibuka katika Kata ya Dodoma Makulu jijini Dodoma na kuwasumbua wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Toufiq ametoa kauli hiyo leo tarehe 13 Juni, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akiuliza swali la nyongeza ambapo amesema kumeibuka kikundi hicho kinachoumiza wananchi.

“Mheshimiwa Naibu Spika kumeibuka kikundi kinachoitwa Panya kalowa ambacho kinaumiza watu, nataka kujua Serikali inachukua hatua gani kudhibiti kikundi hicho ambacho ni hatari kwa wananchi,” amehoji Toufiq.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amesema Serikali inazo taarifa kuhusu kikundi hicho na makundi mengine na tayari wameanza kuwashughulikia.

Amesema tayari kuna baadhi ya vijana ambao wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma wakitokea maeneo hayo lakini kazi zaidi inafanyika kuwabaini wahusika wote.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na polisi katika kuwapatia taarifa sahihi ili kuwabaini vijana wote kwenye makundi hayo.

Hivi karibuni kuliibuka kundi la vijana maarufu Panya Kalowa katika jiji hilo, na kuetekeleza vitendo vya kihalifu kama ukabaji na mauaji yanayoripotiwa katika maeneo kadhaa ya Jiji la Dodoma.

error: Content is protected !!