Friday , 9 June 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Pangua pangua ya Rais Magufuli, ilianzia siku ya kwanza ya kuingia Ikulu 
Habari za SiasaTangulizi

Pangua pangua ya Rais Magufuli, ilianzia siku ya kwanza ya kuingia Ikulu 

Rais John Magufuli
Spread the love

RAIS John Magufuli, amebakiza mwaka mmoja na ushei kukamilisha ngwe yake ya kwanza ya miaka mitano. Akibahatika aweza kuendelea kuhudumu katika kipindi kingine cha miaka mitano, kama rais wa Jamhuri ya Muungano. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Pamoja na kwamba Rais Magufuli amekaa Ikulu, tokea Novemba 2015 na amekuwa serikalini tangu kipindi cha uongozi wa Benjamin Mkapa, bado mpaka sasa, naendelea kupanga safu yake ya uongozi ikiwemo baraza lake la mawaziri.

Kuthibitisha kuwa “bado anapanga safu yake ya uwaziri,” tarehe 8 Juni 2019, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa waziri wake wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, mbunge wa Sikonge, mkoani Tabora.

Nafasi ya Kakunda, imechukuliwa na mbunge wa Karagwe, mkoani Kagera, Innocent Bashungwa. Rais ametangaza kutengua pia uteuzi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere. Nafasi ya Kichere, imekabidhiwa kwa Edwin Mhede, aliyekuwa naibu katibu mkuu wizara ya viwanda.

Rais Magufuli alitangaza baraza lake la mawaziri la kwanza, Desemba 2015. Lilikuwa na mawaziri 19 na manaibu mawaziri 15.Alisema, baadhi ya wizara alikuwa hajateuwa. Alizitaja kuwa ni wizara ya mambo ya ndani, viwanda, ulinzi na katiba na sheria.

Kati yao hao, wanawake walikuwa sita. Alijitapa kuwa baraza hilo, lilikuwa dogo ukilinganisha na mtangulizi wake, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Aliahidi kuunda baraza dogo la mawaziri ili kuwaondolea mzigo wananchi.

Hata hivyo, haikuchukua muda, alifanyia mabadiliko kadhaa baraza lake hilo, kwa kuwahamisha baadhi ya mawaziri huku wengine akiwaondoka katika utumishi wake. 

Pamoja na madai kuwa serikali ilikuwa ndogo, lakini kuwapo kwa makatibu wakuu wawili hadi watatu kwenye wizara moja, kulizidi kuthibitisha kuwa serikali yake, siyo ndogo kama inavyoelezwa.

Ukubwa wa baraza la mawaziri ulizidi kuongezeka, kutoka wizara 18 hadi kufikia wizara wizara 21, kabla ya baadaye kuongezeka na kufikia takribani wizara 30.

Miongoni mwa mabadiliko yaliyoongeza wizara, ni pamoja na hatua ya kuimega wizara ya nishati na madini na kuzifanya wizara mbili – Nishati inayoshughulikia umeme na nyingine inayoshughulikia Madini.

Aidha, wizara ya kilimo, uvuvi na mifugo, iligawanywa na kuundwa wizara mbili – Kilimo iliyobaki na jukumu la kusimamia kilimo, utafiti na pembejeo na nyingine inayoshughulikia mifugo na uvuvi.

Vilevile, tarehe 8 Januari mwaka huu, rais aliunda wizara mpya ya Uwekezaji. Akamteuwa Angellah Kairuki, kuwa waziri. Kabla ya uteuzi huo, Kairuki alikuwa waziri wa nishati.

Licha ya mabadiliko hayo, kuna mawaziri takribani nane walioteuliwa tangu katika baraza la kwanza la mawaziri, hawajawahi kutenguliwa; na au kubadilishiwa.

Miongoni mwao, ni pamoja na January Makamba, Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira; Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu na naibu waziri wake,  Anthony Mavunde.

Wengine, ni Dk. Hussein Mwinyi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; William Lukuvi,  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Ummy Mwalim, waziri wa afya, maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto; Angelina Mabula, naibu wa wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Dk. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, hakuwamo katika uteuzi wa kwanza wa baraza la mawaziri uliotangazwa na rais, tarehe 10 Desemba 2015. Dk. Mpango alitangazwa kushika nafasi hiyo, tarehe 23 Desemba 2015.

Mawaziri waliobadilishiwa wizara waliokuwamo katika baraza la kwanza la Rais Magufuli, ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,  Prof. Makame Mbarawa, ambaye kwa sasa ni wa waziri wa maji na umwagiliaji.

Kabla ya kuwa waziri wa ujenzi, Mbarawa aliteuliwa kuwa waziri wa maji, nafasi ambayo hakuwahi kuitumikia.

Naye Angela Kairuki, alikuwa Waziri Ofisi ya Rais (Utawala Bora), kwa sasa ni waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji. Kabla ya kupelekwa hapa alikuwa waziri wa nishati.

Selemani Jaffo alikuwa naibu waziri ofisi ya rais (TAMISEMI). Hivia sasa, ni waziri kamili wa wizara hiyo.

Aliyekuwa naibu waziri ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), katika baraza la kwanza la mawaziri lililotangazwa na Rais Magufuli, Desemba 205, Luhaga Mpina, ameendelea kubaki ndani ya serikali hiyo. Kwa sasa, Mpina, ni waziri wa mifugo na uvuvi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwele, alikuwa naibu waziri wa maji na umwagiliaji. Kwa sasa, Kamwene, ni waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.

Wengine waliobadilishwa, ni Dk. Medard Kalemani, aliyekuwa naibu waziri wa nishati na madini. Kwa sasa, Kalemani, ni waziri wa nishati.

Dk. Harrison Mwakyembe alibadilishwa kutoka wizara ya katiba na sheria kwenda wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo.

Naye Balozi Augustine Mahiga, alihamishiwa wizara ya katiba na sheria akitokea  wizara ya mambo ya nje. 

Dk. Hamis Andrea Kigwangalla, alikuwa naibu waziri afya lakini kwa sasa ni waziri maliasili na utalii.

Waliotoka kabisa katika baraza la mawaziri la Magufuli aliloliunda Desemba na baadaye kulifanyia mabadiliko miezi michache iliyofuata, ni George Simbachawene, aliyekuwa waziri ofisi ya rais (TAMISEMI); Dk. Abdallah Possi, aliyekuwa naibu waziri ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.

Katika baraza la kwanza la mawaziri la Magufuli, Mwigulu alikuwa waziri wa kilimo, mifugo na uvuvi. Baadaye akapelekwa wizara ya mambo ya ndani  ya nchi. 

Wengine, ni Charles Kitwanga aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani; Charles Mwijage aliyekuwa waziri wa viwanda na biashara na uwekezaji na Nape Nnauye, aliyekuwa waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo.

Mwingine aliyeng’olewa alikuwa mteule wa kwanza wa Rais Magufuli kwenye serikali, Geoger Masaju, ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ndiyo mtu wa kwanza anayeteuliwa na rais kabla ya kuundwa kwa serikali.

Lakini kuna hili pia: Tabia ya Rais Magufuli, kupangua watendaji wake serikalini, haikunza katika mabadiliko ya juzi. Ilianza siku za kwanza kufika Ikulu.

Kuna baadhi ya watu wanadai kuwa mara baada ya rais kuingia Ikulu, aliamua kuwafuta kazi ama kuwaweka pembeni wasaidizi wake waliokuwa wakifanya kazi na mtangulizi wake – Jakaya Mrisho Kikwete.

Baadhi ya wanaotajwa, ni Salva Rweyemamu, aliyekuwa mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais (Ikulu) na Premy Kibanga, aliyekuwa Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Ikulu. Salva aliondoka Ikulu, Novemba 2015.

Hakuna taarifa juu ya Premy kama bado yuko Ikulu au ameshandoka. Lakini tangu kuondoka kwa Salva, mwanahabari huyo aliyewahi kulifanyia kazi shirika la utangazaji la Uingereza (BBC), hajasikika katika taarifa zozote zinazotoka Ikulu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaTangulizi

Ngoma bado mbichi mkataba wa Bandari

Spread the love  SAKATA la mkataba wa uendeshaji, uendelezaji na uboreshaji wa...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mkataba unaweza kuvunjwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mikataba ya utekelezaji bado haijasainiwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

Habari za Siasa

Lussu: Mkataba wa DP bandarini si wa miaka 100

Spread the loveMAKAMU Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amesema hakuna ukweli wowote...

error: Content is protected !!