HUENDA tarehe 5 Januari 2023, ikawa ni siku chungu kwa Kamishna Diwani Athuman, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutengua uteuzi wake ikiwa ni siku mbili tu tangu amteue kuwa Katibu Mkuu Ikulu baada ya kumtoa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), na kuendelea kuifanya safari yake ya uongozi kuwa yam ilima na mabonde. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Katika kipindi cha takribani miaka nane (2015-2023), Kamishna Diwani amehudumu katika nyadhifa nne tofauti ambazo zikikuwa ni kupanda na kushuka kutoka kuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Katibu Tawala Mkoa wa Kagera (RAS), Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) hadi Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Katibu Mkuu Ikulu na sasa haijulikani atakwenda wapi juu au chini au atasalia ndani ya jeshi la Polisi.
Jina la Kamishna Diwani lilizidi kupata umaarufu 2015 baada ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, kumteua kuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), kabla ya uteuzi huo alikuwa Kaimu Kamishna wa Kamisheni ya Inteljensia ya Jinai.
Soma zaidi:-
-
Samia amtumbua Balozi wa Tanzania UN, apangua safu TISS, Ikulu
-
Diwani ang’olewa Ikulu kabla ya kuapishwa
Kamishna Athumani aliendelea katika wadhifa huo mpaka kwenye Serikali ya Awamu ya Tano, hadi Novemba 2016, baada ya aliyekuwa Rais wa awamu hiyo, Hayati John Magufuli, kumng’oa na kumteua kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kagera.
Baada ya safari ya uongozi ya Kamishna Diwani kushuka, ilipanda tena Septemba 2018, baada ya Rais Magufuli kumteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Mwaka mmoja baadae, Septemba 2019, Hayati Magufuli alimteua Kamishna Diwani kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), akichukua nafasi ya Dk. Modestus Kipilimba.
Kamishna Diwani alihudumu katika wadhifa wa Ukurugenzi wa TISS kwa muda wa zaidi ya miaka miwili, tangu Septemba 2019 hadi Januari 2023.
Licha ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ikulu, Kamishna Diwani hajafanikiwa kuhudumu kwenye wadhifa huo kutokana na uteuzi wake kutenguliwa kabla hajaapishwa, ikiwa zimepita siku mbili tangu kuteuliwa.
Mbali na nyadhifa hizo, Kamishna Diwani aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Jeshi la Polisi kabla ya 2015, ikiwemo msaidizi binafsi wa aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Omary Mahita na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya.
Leave a comment