SERIKALI ya Palestina, imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), iwachunguze maafisa wa Serikali ya Israel wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Wito huo umetolewa na Ubalozi wa Palestina nchini Tanzania baada ya Ripoti ya Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW), kubainisha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya maafisa wa Serikali ya Israel.
“Ubalozi wa Palestina unapenda kutoa msimamo wa Serikali ya Palestina kukaribisha ripoti ya HRW, juu ya uhalifu wa Israeli dhidi ya ubinadamu, ubaguzi wa rangi na mateso, ikiitaka ICC ichunguze maafisa wa Israeli wanaohusishwa na uhalifu huu,” imesema taarifa ya Ubalozi wa Palestina.
Taarifa ya ubalozi huo imesema, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina, imesema vitendo hivyo vinavyofanywa na utawala wa Israel vinaathiri maisha ya Wapalestina, hasa kufuatia hatua yake ya kuendelea kuchuku ardhi ya Taifa hilo.
“Ripoti hiyo imefichua hali ya ukoloni wa Israeli kama serikali iliyokita mizizi ya ukuu wa Kiyahudi na utawala juu ya watu wa Palestina na uongezekaji wa makazi haramu katika eneo la Palestina na hivyobasi kuathiri kila sehemu ya maisha ya Wapalestina,” imesema Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina.
Kufuatia vitendo hivyo, Ubalozi wa Palestina nchini Tanzania, umezitaka Jumuiya za Kimataifa kuingilia kati vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, vinavyofanywa na utawala wa Israel dhidi ya raia wa Taifa hilo.
“Ubalozi pia unakumbusha Mataifa na viongozi wa mataifa mbalimbali kuwa uhalifu wa ubaguzi wa rangi ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa. Hivyo basi, mataifa na jamii ya kimataifa lazima ichukue hatua za haraka na madhubuti kulazimisha kukomeshwa kwa utawala wa kibaguzi wa Israeli,” imesema taarifa ya ubalozi huo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Serikali ya Israel inatuhumiwa kukandamiza mifumo ya uongozi wa Wapalestina, pamoja na kuzuia harakati zao za kudai ardhi yao iliyotwaliwa na Waisrael.
Ripoti ya HRW imekuja miezi mitatu baada ya kuchapishwa kwa ripoti ya Shirika la Haki za Binadamu la Israeli (B’Tselem), ambayo pia iliishutumu Israeli kuwa serikali ya ubaguzi wa rangi na isiyofuata misingiya kidemokrasia kama inavyojinasibu ulimwenguni.
Leave a comment