WAZIRI Mkuu wa Pakistani, Imran Khan ameuonya uongozi mpya ya Afghanistan kuunda haraka Serikali shirikishi ili kuzuia uwezekano wa kuibuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Anaripoti Helena Mkonyi, TUDARCo … (endelea).
Akizungumza na BBC katika mahojiano maalumu, Waziri Mkuu huyo amesema kundi la wanamgambo wa Taliban ambalo limefanikiwa kuchukua madaraka huko Afghanistan linatakiwa kushirikisha wananchi katika kuunda serikali mpya ili kuungwa mkono na mataifa mengine duniani.
Khan amesema machafuko yoyote yanayoweza kutoka Afghanistan yataiweka Pakistan katika hali ya hatari hasa ikizingatiwa ni nchi majirani na washirika wa siku nyingi.
Serikali ya Pakistani ambayo ina mfungamano wa siku nyingi na viongozi wa Taliban pia imetoa wito kwa viongozi wa mataifa yenye nguvu duniani kuunga mkono mabadiliko yaliyokea huko Afghanistan.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 10 sawa na Sh trilioni 23.1 zimezuiliwa katika benki kuu ya Afghanistan huku Benki kuu ya Marekani ikitajwa kuwa na mkono wa shinikizo kuhusu akiba hiyo ya fedha.
Mapema wiki hii Waziri wa Mambo ya nje wa Pakistani, Shah Mahmood Qureshi alitoa wito kwa Marekani kuachia fedha hizo ili kunusuru huduma za kijamii ndani ya Afghanistan ambazo zimedorora.
Leave a comment