July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Padre Mapunda ateuliwa kuwa Askofu Singida

Papa Francis

Spread the love

BABA Mtakatifu, Francis, amemteua Padre Edward Mapunda kutoka Jimbo Katoliki la Singida kuwa Askofu mpya wa jimbo hilo. Anaandika Josephat Isango (endelea).

Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Mapunda alikuwa ni mchumi na Mratibu wa Idara ya Afya jimbo.

Askofu mteule Mapunda alizaliwa tarehe 30 Septemba 1964, huko Mango katika Jimbo Katoliki la Mbinga. Baada ya masomo ya Sekondari kwenye Seminari ya Dung’unyi – Singida, aliendelea na masomo ya kidato cha tano na sita kwenye Seminari ndogo ya Rubya, Jimbo Katoliki Bukoba.

Amepata masomo ya Falsafa katika Seminari kuu ya Ntungamo iliyoko Jimbo Katoliki Bukoba na baadaye akahamia Seminari kuu ya Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa masomo ya taalimungu.

Baada ya safari hiyo ndefu ya majiundo ya kikasisi, hatimaye tarehe 23 Novemba 1997, alipewa daraja takatifu la upadre, jimboni Singida.

Tangu wakati huo, Askofu mteule Mapunda alifanya shughuli zifuatazo: Kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2000, alikuwa ni mlezi wa Seminari ndogo ya Dung’unyi. Mwaka 2000 – 2004 alijiendeleza kwa masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata Shahada ya Uzamili katika elimu.

Kati ya mwaka 2004 hadi 2006, alikuwa ni makamu Gombera wa Seminari ndogo ya Dung’unyi na kuanzia mwaka 2006 hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu mpya wa Singida, alikuwa ni mchumi na mratibu wa Idara ya Afya jimbo.

Jimbo Katoliki Singida ni sehemu ya Jimbo Kuu la Dodoma ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 49, 341 na wananchi zaidi ya 1, 500, 000, ambao kati yao Wakatoliki ni 238, 307.

 Jimbo Katoliki Singida lina Parokia 22, zinazohudumiwa na mapadre 67 kati yao 50 ni wa jimbo na 17 ni wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume.

Wapo pia watawa 423 na majandokasisi 14 katika jimbo hili ambalo limekuwa wazi tangu tarehe 13 Januari 2013, baada ya Askofu wake, Desiderius Rwoma kuteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba.

error: Content is protected !!