KATIBU Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padre Charles Kitima amewataka viongozi wa dini kukemea dhambi zinazojitokeza katika chaguzi, ili kuhakikisha zinakuwa za haki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Padre Kitima ametoa wito huo leo tarehe 17 Novemba 2023, akitoa mrejesho wa ziara ya baadhi ya viongozi wa dini kwenda kujifunza namna ya kutenda haki kwenye uchaguzi, katika nchi zilizofanikiwa katika masuala hayo, ikiwemo Kenya na Afrika Kusini.
Kiongozi huyo wa dini amedai kuwa, imefika mahali baadhi ya viongozi wa dini wanaona makosa au dhambi zinazofanyika katika chaguzi, kama sio chukizo mbele za Mungu.

“Na kwenye uchaguzi Tanzania imefika mahali viongozi wa dini sijui kama mtalionaje, ni kama dhana ya dhambi inafutwa kabisa kwenye mambo ya siasa. Yaani unaweza kufanya tendo ambalo si zuri kwenye siasa na ikaonekana si dhambi havimchukizi Mungu,” amesema Padre Kitima.
Akizungumzia ziara ya viongizi wa dini nchini Kenya, Padre Kitima amesema walifanikiwa kujifunza masuala mbalimbali ambayo amedai hapa hayapo, ikiwemo tume ya uchaguzi nchini humo kuaminika mbele ya wananchi, kutenda haki kwa wagombea wa pande zote, pamoja na kuwaandaa wananchi kushiriki uchaguzi.
Leave a comment