Tuesday , 23 April 2024
Home Habari Mchanganyiko PAC yaridhishwa na uwekezaji Bandari Dar
Habari Mchanganyiko

PAC yaridhishwa na uwekezaji Bandari Dar

Spread the love

 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) nchini Tanzania, imesema uwekezaji wa zaidi ya Sh.1 trilioni uliofanywa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kwenye Bandari ya Dar es Salaam umeonesha tija na mafanikio makubwa. Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa jana Jumanne tarehe 22 Machi 2022 na Makamu Mwenyekiti wa PAC, Japhet Hasunga wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea Bandari ya Dar es Salaam na kuona uwekezaji uliofanywa hadi sasa.

Hasunga alisema taarifa waliyopewa inaonesha ufanisi wa bandari umeongezeka hali ambayo inachangia kuongeza mapato.

“Tumezungumza na menejimenti ya TPA na kutembelea maeneo ya uwekezaji kimsingi tumeridhishwa na maboresho yanayofanyika, tunawataka waongeze kasi ya usimamizi,” alisema.

Makamu Mwenyekiti huyo alisema uwekezaji wa takribani Sh.1 trilioni umekuwa na tija katika baadhi ya maeneo ambapo matarajio yao ni kuona faida kubwa baada ya maboresho kukamilika.

Hasunga alisema kupitia uwekezaji huo Tanzania imeweza kupokea meli kubwa ambazo zinaingiza shehena nyingi za mzigo hivyo kuongeza mapato ya nchi.

Alisema ufanisi umeongezeka kwenye upakuaji wa shehena za mizigo kutoka siku 10 hadi siku tatu jambo ambalo ni la kupongezwa.

“Bandari ni taasisi nyeti kwenye kukusanya mapato, hivyo tunaomba Serikali kuongeza kasi ya uboreshaji Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza mapato na kukuza uchumi,” amesema.

Makamu mwenyekiti huyo aliipongeza TPA kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuboresha utendaji na ufanisi wa TPA.

Alisema kamati imeridhishwa na matumizi ya mifumo ya kisasa kwenye kuhudumia wateja jambo ambalo linaokoa muda na kuepusha upotevu wa mapato ya Serikali

Hasunga alisema pamoja na juhudi zinazofanyika kuongeza wigo wa masoko Kamati imeilekeza Menejimenti ya TPA kutafuta masoko zaidi katika nchi zote jirani kama DR Congo, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na Sudani Kusini, hali ambayo itawezesha kuongeza mapato ya Mamlaka na nchi kwa ujumla.

Aidha, Hasunga aliitaka TPA kuhakikisha mitambo mipya inawasili kwa wakati ili kuongeza uzalishajiu.

“Pia tumewashauri washirikiane na wenzao wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuhakikisha huduma hizo zinakuwepo mradi ukikamilika,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TPA, Balozi Ernest Mangu alisema mamlaka imechukuwa maelekezo ya kamati kuhakikisha bandari zote zinakuwa na tija.

“Sisi tunajipanga kuhakikisha maboresho makubwa yanafanyika kwenye bandari zetu kwa kila mtu kujituma,” alisema Mangu aliyewahi kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi alisema mamlaka inaendelea kutekeleza mradi hatua kwa hatua ili ikamilike kwa wakati.

Hamissi alisema mradi wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ( DMGP) umeanza mwaka 2017 na unatakiwa kukamilika mwaka 2024, kama ulivyopangwa.

“Mradi huu unatakiwa kukamilika 2024 na hili ndilo tunalipigania ili kuepusha gharama kuongezeka,” alisema.

Hamissi alisema mradi wa DMGP unahusu kuchimba kuboresha Gati Na. 1-7 kwa kuongeza kina cha gati kufikia mita 14.5, kujenga Gati jipya la magari (RO-RO), na kuchimba kina cha lango Bandari la kuingilia meli kufikia mita 15.5 na kuongeza mzunguko wa kugeuzia meli, kazi inayoendelea.

Hamissi alisema katika awamu nyingine ya Mradi TPA itatoa mafunzo kwa wafanyakazi wake ili kuwajengea uwezo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari Mchanganyiko

DC ampongeza Dk. Rose Rwakatare kwa kusaidia waathirika wa mafuriko Mlimba

Spread the loveMWENYEKITI wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk.  Rose Rwakatare...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

error: Content is protected !!