October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Othman ala kiapo kutimiza ndoto ya Maalim Seif

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othuman Masoud Othuman

Spread the love

 

MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman, amekula kiapo cha kutimiza ndoto ya mrithi wake, Maalim Seif Shariff Hamad ya kurejesha mamlaka kamili Visiwani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar…(endelea).

Othman ametoa msimamo huo jana tarehe 2 Oktoba 2021, katika ziara yake Visiwani Unguja.

Makamu huyo wa kwanza wa Rais Zanzibar, alisema Maalim Seif alikuwa na dhamira na nia ya kurejesha mamlaka ya visiwa hivyo, kama ilivyokuwa kabla haijaungana na Tanganyika.

“Imani ni amana na amana ada yake ni kuirejesha nami nitairejesha vizuri zaidi, naomba niwaahidi mmeniamini na mimi nitarejesha amana hii kadri ya uwezo wangu, ukweli tumeondokewa Mungu alitupa mzee wetu Maalim kama wakfu na hidaya, kwamba aje atutumikie,” alisema Othman.

Othman alisema “kwa vile ambavyo analijua yeye tumekuwa kwenye madhila haya muda mrefu, sitaki kurudia historia ya nchi hii, hili ndilo linanipa moyo zaidi kwamba  Zanzibar hatuzungumzi kama inavyozungumzwa leo na baadhi yetu wasiojuia thamani ya nchi yao.”

Alisema, Zanzibar ilikuwa dola kabla nchi nyingi za Afrika hazijaanzishwa, huku akikumbushia namna ilivyokuwa na Ubalozi wa Marekani 1837 na Ubalozi wa Uingereza 1941.

“Sasa kukapitishwa pitishwa ghiliba na siasa tukaambiwa wewe haujulikani, aliyekuwa mgeni leo ana haki zaidi. Nchi ilikotoka tulitegemea iwepo mbali sana, sisi sio wa kuzungumza leo kujilinganisha na nchi yeyote Afrika,”

“Lakini mimi si Maalim, lakini jambo moja ambalo ninalo ni kwamba, zile dhamira na nia alizokuwa nazo kiongozi wetu akisimamia, basi na mimi nitajitahidi ndiyo maana mkanipa imani. Katika hilo sitorudi nyuma kwa sababu yapo ambayo tunapaswa tuyafikie hatujayafikia,” alisema Othman.

Aidha, Othman alisema ili Zanzibar ipate maendeleo inatakiwa iwe na mfumo mzuri wa kikatiba pamoja na tume huru ya uchaguzi.

“Tunachotaka tupate mfumo wa katiba ambayo itatuwezesha tuwe huru kufanya chaguzi, tuchague nani tunayemtaka. Hilo ni la lazima,” alisema Othman.

Othman aliteuliwa na chama chake kisha kuthibitishwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais visiwani humo, tarehe 1 Machi 2021.

Baada ya Maalim Seif kufariki dunia tarehe 17 Februari, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu.

error: Content is protected !!