August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Omar Mzee sasa Balozi

Omar Yussuf Mzee

Spread the love

 

KADA maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Omar Yussuf Mzee, aliyetoa mchango mkubwa katika mbinu zilizokiwezesha chama hicho kubaki madarakani upande wa Zanzibar, mwaka 2010, ameteuliwa Balozi, anaandika Jabir Idrissa.

Mzee ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya maendeleo ya takwimu mwenye shahada ya uzamili (Shahada ya Pili), ambaye ameteuliwa balozi katika uteuzi wa mabalozi 15 uliofanywa na Rais John Magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dar es Salaam, Mzee ni mmoja wa mabalozi wapya ambao watatangaziwa vituo vyao vya kazi baadae.

Mzee amebaki nje ya serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein ambaye baada ya kutangazwa mshindi wa urais wa Zanzibar kufutia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010, alimteua Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango.

Hapo alikuwa ndiye waziri wa kwanza wa wizara hiyo katika serikali mpya iliyokuwa chini ya mfumo wa umoja wa kitaifa – Government of National Unity (GNU) iliyoundwa na Dk. Shein.

Mzee anafahamika kuwahi kutumikia nafasi ya katibu mkuu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa muda mrefu, kabla ya 2005 alipopata ubunge wa kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, nafasi iliyomwezesha kuteuliwa kuwa naibu waziri wa Ulinzi na Jeshi la KUjenga Taifa.

Mwaka 2008 katika mabadiliko ya baraza la mawaziri, Rais Kikwete alimhamishia kwa nafasi hiyo ya unaibu waziri katika Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango.

Wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010, alishirikishwa katika kikosi kilichoshughulikia takwimu za uchaguzi ndani ya Ofisi Kuu za CCM Kisiwandui, na hatimaye kuwezesha CCM kung’ang’ania madarakani.

Ni katika uchaguzi huo, CCM iliyomsimamisha Dk. Shein kuwa mgombea wake wa urais, ilishikilia kiti hicho na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) chini ya mwenyekiti wake Khatibu Mwinchande, ikamtangaza mshindi.

Mzee ambaye alionekana kada mwenye uhusiano wa karibu na Dk. Shein kwa wakati wote wa 2010/2015, hakuteuliwa katika serikali ya sasa, yenyewe ikiwa imepatikana kwa mbinu zilezile za kuhujumu uchaguzi.

Fununu kutoka ndani ya CCM zimekuwa zikidai kuwa hapendezi kwa kundi jingine la makada waliosimamia hujumu ya safari hii kwenye uchaguzi wa 25 Oktoba 2015.

Baada ya kumaliza elimu ya juu ya sekondari Chuo cha Lumumba, Mzee alichukua kozi ya shahada ya takwimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikohitimu mwaka 1982, akajiunga na Chuo Kikuu cha Taifa Australia alikohitimu shahada ya pili mwaka 1985 na mwaka 1988 akahitimu stashahada ya uzamili Chuo Kikuu cha Nehru, India.

 

error: Content is protected !!