August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ole Sendeka aanza porojo za Nape, Kinana

Spread the love

CHRISTOPHER Ole Sendeka, Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameanza porojo za Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM na Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa chama hicho, anaandika Christina Raphael.

Akifungua mafunzo ya siku mbili kwa madiwani na viongozi wakuu wa CCM katika kata zote za Manispaa ya Morogoro leo, Ole Sendeka amemwomba Rais John Magufuli kuanika hadharani majina ya wakwepa kodi ya mafuta na kuwachukulia hatua.

Pia waliosababisha kuwepo kwa matawi ya mabomba ya mafuta ya magari katika Bandari Kuu ya Tanzania (TPA) hivyo kujipatia fedha nyingi kwa njia haramu.

Ole Sendeka anasema hayo huku akijuwa kwamba, serikali inatambua kuwepo kwa majina hayo na haipo tayari kuyaweka hadharani.

Tabia hii walikuwa nayo Nape na Kinana miaka miwili iliyopita ambapo walituhumu watendaji wabovu na mawaziri mizigo ndani ya serikali huku Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete ikiendelea kuwabeba. Tuhuma hizo walizitoa majukwaani.

Katika mafunzo hayo Ole Sendeka ameonesha kwamba, ndani ya TPA kuna vigogo ambao hawajachukuliwa hatua, hivyo anapaswa ‘kuwatumbua’ hadharani kama ambavyo amefanya kwa watumishi wengine wa umma.

Amedai, kwa kuanika majina hayo Watanzania wanaweza kurejesha imani kwa chama na serikali yake huku akiwataka wana CCM kumuunga mkono.

Amesema, Rais Magufuli anapaswa kupiga hatua mbele zaidi TPA kwa kuanika majina ya watu hao ili kujengea heshima CCM.

‘’Mimi nimeamua kumuunga mkono Rais hata akimtumbua ndugu yangu wa tumbo moja, na nyie nawaomba hata kama ndugu yako anatumbuliwa, inabidi uvumilie na umuunge mkono ili aweze kufanya kazi yake vizuri na kuleta manufaa kwa wananchi walio wengi,’’ amesema na kwamba, hakuna mtu yeyote anayeogopwa katika Serikali ya Rais Magufuli.

“Lazima tuifanye CCM iwe kimbilio la wanyonge, chama kirudi katika uasili wake, kazi anayofanya Magufuli sio tu ya kufanya CCM iendelee kushinda mwaka 2020, bali pia anaweka msingi wa kuasisiwa’’ amesema.

Pia amewataka viongozi wa CCM kuacha makundi badala yake, wawachukulie hatua wale waliosatiti chama hicho wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu.

“Wakati wa mchakato wa urais kila mmoja alikuwa katika kambi yake, na baada ya uchaguzi wote wanatakiwa kuwa pamoja, sasa wapo viongozi ambao wanatumia kigezo hicho kuwahukumu watu ambao wanajua ni tishio kwao wanapotaka kugombea, hiyo sio sahihi,’’ amesema.

Kulwa Milonge, Katibu wa CCM Wilaya ya Morogoro amesema, katika kuhakikisha chama kinafuata nyayo za Rais Magufuli, wameweka utaratibu wa kusikiliza kero za wanachama siku moja katika wiki na kuzifanyia kazi.

Pia amesema, ili kumuunga mkono Rais katika harakati zake za kuboresha elimu, CCM wilaya imeandaa mkakati wa kutafuta madawati 4000 kwa ajili ya kusaidia Shule za Manispaa ya Morogoro.

Fikiri Juma, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo viongozi hao ili kuweza kufanya kazi zao kwa ufasaha.

error: Content is protected !!