August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ole Nangole aja juu

Spread the love

IKIWA zimepita siku chache baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kumvua Ubunge wa Jimbo la Longido, Onesmo ole Nangole, sasa amekata rufaa, anaandika Faki Sosi.

Nangole kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alitangazwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kwenye uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana.

Hivi karibuni mahakama hiyo imetengua Ubunge wa Nangole kwa madai ya kugubikwa na kasoro kadhaa na kudaiwa kuondoa uhalali wa yeye (Nangole) kuendelea kushikilia nafasi hiyo.

Jaji Sivangilwa Mwangesi wa mahakama hiyo alieleza kuridhishwa kwake na hali halisi katika chumba cha kuisabia kura kwamba haikukidhi matakwa halisi ya uisabuji wa kura.

Hatua ya kumvua ubunge Nangole imekuwa ikipingwa na viongozi pia wanachama wa chama hicho kwamba, haiakisi matakwa ya kisheria na kwamba, jambo hilo halikubaliki.

Hata hivyo Nangole akiwa katika Jimbo la Longido wakati akiwashukuru wananchi wa jimbo hilo amesema kuwa, hakubaliana na hukumu hiyo.

“Nimeishawasilisha maombi ya kukata rufaa” anasema Nangole na kuongeza kuwa, maombi hayo tayari yamepokewa.

Amesisitiza kuwa, madai ya kuwepo kwa mazingira yasiyo rafiki ama kufanya fujo kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayana msingi wowote na kwamba, kilichokuwa kikisimamiwa ilikuwa ni madai ya kusimamiwa kwa haki.

Anasema, hatua hiyo ndiyo iliyowezesha kutangazwa kwa matokeo kama yalivyokuwa yakionesha na kwamba, tayari aliona kuwepo kwa mazingira ya kutaka ‘kuchakachuliwa’ kwa matokeo hayo.

“Kwa hakika hakukuwa na haki hata kidogo katika hukumu,” amesema Nangole.

Kesi ya kupinga ubunge wa Nangole ilifunguliwa na Dk. Stephen Keruswa, aliyekuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 

error: Content is protected !!