January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Oilers hali tete Azam RBA, Savio yashinda

Logo ya Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam

Spread the love

OILERS juzi Jumapili ilishindwa kutamba mbele ya Jogoo baada ya kufungwa pointi 85-79 katika mwendelezo wa michuano ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam ‘Azam RBA’, mechi hiyo ilifanyika Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Matokeo hayo yaliifanya Oilers iendelee kushika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi hiyo kwa kukusanya pointi 9 huku ikibakiwa na mechi moja ya raundi ya kwanza dhidi ya Chui itakayochezwa Ijumaa wakati Jogoo wanashika nafasi sita ikiwa na pointi 14 nao wamebakiza mechi moja dhidi ya Kurasini Heat itakayochezwa Jumamosi.

Kocha mkuu wa Oilers, William Mziray ‘Kigje’ aliliambia MwanaHALISI Online kuwa tatizo kubwa linaloikumba timu yao kupata matokeo mabovu ni kutokuwa na mazoezi ya kutosha kwani wachezaji wake wengi ni wafanyakazi hivyo wanakosa muda wa mazoezi.

“Inasikitisha kupata matokeo kama haya, timu haina mazoezi kabisa wachezaji wangu wengi ni wafanyakazi hivyo huwa tunakutana siku ya mechi tu jambo ambalo ni hatari, naamini mechi zijazo za mzunguko wa pili tutajitahidi kupigana ili tubaki kwenye ligi,” alisema Kigje.

Savio yenyewe ilishinda mechi yao dhidi ya Kurasini Heat kwa pointi 57- 44 na hivyo kushika nafasi ya tano kwenye msimamo ikiwa na pointi 14 wakati Kurasini wao wanashika nafasi nane ikiwa na pointi 11. Savio wamebakiza mechi mbili itakayochezwa Ijumaa na Vijana mechi nyingine watacheza Jumamosi na Mgulani wakati Kurasini watacheza na Jogoo.

Mechi nyingine za kufunga mzunguko wa kwanza zitakazochezwa wikiendi hii ni kati ya Mgulani JKT na Chang’ombe United, Pazi na JKT Stars, DB Lioness na Jeshi Stars, Nayo Chui itaoneshana kazi na DB Young Stars.

error: Content is protected !!