July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ohio wasitisha dawa ya kunyongea

Kitanda cha kunyongea watuhumiwa kwa njia ya sindano ya sumu

Spread the love

MAMLAKA ya Jimbo la Ohio imesitisha matumizi ya dawa mbili mchanganyiko kwa ajili ya kunyonga watu baada ya kusababisha kizaazaa wakati wa kumnyonga Dennis McGuire, Januari 2014.

Dawa zilizopigwa marufuku ni mchanganyiko wa Midazolam na Hydromorphone.

Dawa hiyo ilisababisha mnyongwaji kufariki dunia baada ya muda mrefu tofauti na muda uliozoeleka. Lakini dawa hiyo ilivunja rekodi Arizona ambako ilichukua saa 2 mnyongwaji kupoteza maisha ukiwa ni muda mrefu mno.

Sasa Ohio imependekeza matumizi ya Pentobarbital au Thiopental Sodium na dawa ya usingizi itatumika pia.

Unyongaji mwingine unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao unaweza kuchelewa ili kutafuta kiwanda kitakachotengeneza dawa hizo zilizopendekezwa.

Unyongaji wa  Dennis McGuire

Unyongwaji wa McGuire ulileta mvutano mkubwa na ulizungumziwa sana na vyombo vya habari, kwani  ulikuwa wa mateso makubwa, maumivu na hofu kubwa kwa McGuire.

Pamoja na kosa la ubakaji na uuaji alilolifanya kwa mwanamke mjauzito, McGuire alitetewa kuwa adhabu aliyopewa ya kunyongwa haikuangalia ubinadamu kwa madai alisababishiwa mateso makubwa.

Ohio iliamua kumnyonga kwa kutumia dawa mbili baada ya kampuni kadhaa zilizokuwa zinatengeneza dawa hiyo Ulaya kuacha kufanya hivyo baada ya nchi nyingi za Ulaya kuondoa adhabu ya kifo.

Kwa kukosa dawa moja iliyokuwa inatumika awali iliifanya Ohio itafute mbadala kwa kutengeneza dawa mbili zisizofuata viwango kama majaribio na hivyo kuleta mjadala mkubwa baada ya unyongaji huo kuwa wa aina yake na wa mateso makubwa.

McGuire alipokuwa ananyongwa baadhi ya vyombo vya habari viliruhusiwa kushuhudia huku watoto wake; wa kike na wa kiume na mtoto wa kike wa kufikia wakishuhudia.

Vitendo alivyofanya McGuire wakati ananyongwa

McGuire alianza kwa kufungua kiganja cha mkono wa kushoto na baadaye akakifunga kana kwamba alikuwa anatoa ishara ya kwa heri kwa wanawe.

Baadaye akapandisha mwili wake juu, akaangalia waliko wanawe, na kusema, “Ninawapenda, ninawapenda”.

Baada ya hapo alifungua mdomo bila ya kutoa sauti mara kadhaa huku tumbo lake likipanda juu na kushuka.

McGuire alipaliwa mara kadhaa huku akionyesha kuhangaika kwa kukosa hewa na akionyesha yupo kwenye maumivu makali.\

Kwa kutambua ugumu wa upatikanaji wa dawa hizo kutoka kwa wasambazaji, Gavana John Kasich amesaini mswada ambao utazuia wananchi kupata orodha ya majina ya kampuni zinazotengeneza dawa hizo.

Sheria hii imewafanya wafungwa wanne wanaosubiri kunyongwa kulalamika na kufungua mashtaka kwa kudai sheria hiyo itainyima jamii haki ya kupata habari, ambazo zitafungua mjadala kwa wananchi juu ya adhabu ya kifo.

Marekani ina majimbo 50, kati ya hayo 32 yanatumia sheria ya kifo huku majimbo 18 yamefuta sheria hiyo kwa miaka tofauti. Baadhi ya majimbo yaliyofuta sheria hiyo ya kifo miaka mingi iliyopita ni pamoja na Michigan mwaka 1846, Wisconsin (1853), Maine (1887) nakadhalika.

Mwaka jana wafungwa wapatao 35 walinyongwa. Kwa ujumla tangu mwaka 1976, jimbo la Texas linaongoza kwa idadi kubwa ya wafungwa walionyongwa.

Nchi kumi zinazoongoza kwa utekelezaji wa adhabu ya kifo ni pamoja na China inayoongoza ikifuatiwa na Iran, Saud Arabia, Iraq, USA, Pakistan, Yemen, Vietnam na Libya ni ya kumi, kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binaadamu (Amnesty International).

McGuire alihukumiwa kifo 1994 na kunyongwa mwaka jana kwa kosa la kubaka na kumuua Joy Stewart (22) aliyekuwa mjamzito wa miezi saba.

error: Content is protected !!