October 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

ACT chazidi kupasuka, Prof. Kitila, Mwigamba wawatimua kina Limbu

Katibu Mkuu wa ACT, Samson Mwigamba

Spread the love
UPDATE 12:39

CHAMA cha ACT-Tanzania, kimepasuka. Waliofukuzwa uwanachama, Samson Mwigamba na Prof. Kitila Mkumbo, wamedai kumsimamisha unyekiti wa chama hicho, Kadawi Lucas Limbu. Anaandika Sarafina Lidwino.

Maamuzi ya kumsimamisha Limbu uwanachama yamefikiwa katika kinachoitwa, kikao cha Kamati Kuu (CC), kilichofanyika jijini Dar es Salaam leo.

Mwigamba na Prof. Kitila walifukuzwa kutoka katika chama hicho, 31 Desemba 2013. Kamati ya wajumbe 11 inayotambuwa na Sheria Na. 5 ya vyama vya siasa, ndiyo iliyopitisha maamuzi ya kuwavua uwanachama viongozi hao.

Mbali na Prof. Kitila na Mwigamba, mwingine aliyefukuzwa uwanachama, ni Shaban Mambo, anayejiita makamu mwenyekiti wa chama hicho (Tanzania Bara). Kikao kilikuwa chini ya uenyekiti wa Limbu.

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja siku tatu baada ya Limbu kuamuru kuzifunga kwa komeo, ofisi za chama hicho na kuonya, “Yeyote atakayeingia ndani bila idhini ya mwenyekiti, ni mvamizi na achukuliwe kuwa mhalifu anayetaka kukiibia chama mali zake.”

Prof. Kitila, aliyefukuzwa Chadema na kukimbilia ACT-Tanzania kinachodaiwa kuongozwa “kinyemela” na Zitto Kabwe, anaponzwa na tuhuma za “kuhujumu chama” na kushiriki maandalizi ya kufanya “mapinduzi” ya kumwondoa mwenyekiti wa sasa Kadawi Limbu ili Zitto aweze kushika usukani wa chama hicho.

Zitto, ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, alifukuzwa Chadema yapata mwaka mmoja sasa, na tangu hapo amekuwa akifahamika kuwa mwanzilishi au “mwanachama wa kimyakimya” wa ACT.

Tayari kuna kambi mbili katika uongozi wa ACT – moja ya wajumbe wanaokubaliana na ujio wa Zitto kuwa mwenyekiti; na nyingine inayotaka Zitto aje akiwa mwanachama wa kawaida.

Hata hivyo, taarifa zinasema, Prof. Kitila, Mwigamba na Mambo, siyo wanachama halali wa ACT – Tanzania. Kadi ambazo wamejipa siyo kadi halisi.

“…hawa watu hawakutaka kujiunga na chama chetu. Walitaka kuanzisha chama ndani ya chama. Ndiyo maana wakajipa kadi zao, wakaandika katiba yao, nembo yao na sasa wanataka kuteka chama na kisha kukibadili jina. Hatutakubali kukiacha chama tulichopigania kifie mikononi mwa wahamiaji. Tumejipanga kukabiliana nao,” ameeleza Limbu.

Kundi la wanachama 11 ndilo linaongoza chama, akiwemo mwenyekiti, makamu wake na katibu mkuu. Hata hivyo, nao hawajachaguliwa rasmi na kuwa na kamati kuu kama katiba yao inavyoelekeza.

Mtoa taarifa mwingine amelieleza gazeti hili kuwa Shaaban Mambo, ambaye ni makamu mwenyeiti wa sasa, amekuwa akisikika akisema kuwa “Limbu ni mwenyekiti boya,” na kwamba mwenyekiti halisi anatarajiwa kuwasili “…mapema mwaka huu.”

Wakati kundi hilo moja likipanga kupangua mipango ya kumsimika Zitto; nao Kitila na Mwigamba wanadaiwa kuitisha “kikao cha Kamati Kuu” chenye lengo la kuwafukuza wale ambao wanapinga “ujio” wa Zitto.

Mtoa taarifa amesema, “Mwigamba ameitisha kikao kinyume cha katiba. Yeye na wenzake wamepanga kuutumia mkutano huo kuwafukuza baadhi ya viongozi; wakiwemo mwenyekiti wa sasa na wale wasiokubaliana nao.”

Amesema, Mwigamba na Kitila wanataka kuteka ATC; wanawagawa wanachama na sasa wanapanga mkakati wa kumfukuza mwenyekiti (Limbu), ili kumkabidhi Zitto chama.

Habari ya awali

MWENYEKITI wa chama cha ACT-Tanzania, Lucas Limbu, amezifunga kwa komeo, ofisi za chama hicho zilizoko Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
Mbali na kuzifunga ofisi hizo, Limbu amemuandikia mkuu wa jeshi la polisi kuwa ofisi za chama hicho zimefungwa kwa kile alichoita, “kuzuia uhalifu.”
Ameongeza, “Yeyote atakayeingia ndani ya ofisi hiyo bila idhini ya mwenyekiti, ni mvamizi na achukuliwe kuwa mhalifu anayetaka kukiibia chama mali zake.”
Aidha, Limbu amewasilisha kwa msajili wa vyama vya siasa, nyaraka za uthibitisho wa kufutwa uwanachama Pro. Kitila Mkumbo, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Samson Mwigamba, aliyekuwa katibu mkuu na Shaban Mambo, aliyekuwa akijitambulisha kuwa makamu mwenyekiti. Anaripoti Pendo Omary.
Habari zaidi, MwanaHALISI Online, Jumatatu.
error: Content is protected !!