July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ofisi ya Msajili kukesha kusubiri fomu za gharama

Spread the love

VYAMA vya siasa nchini vimekumbushwa kurejesha ripoti ya gharama za uchaguzi kwa kuwa mwisho wa kurejesha ni kesho na kwamba ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itakuwa wazi licha ya kuwa ni siku ya mapumziko, anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya siasa nchini amesisitiza kuwa endapo itatokea kuna chama kisichorejesha ripoti kwa wakati sheria itachukua mkondo wake.

“Tunasisitiza watu wasifanye kazi kwa mazoea kama mwanzo walikuwa hawapelekwi mahakamani wakati huu tutawapeleka, hicho ndicho labda ndiyo mnachoweza kuwaambia kwamba wakati huu tutafanya jinsi sheria ilivyo,” amesema.

Piencia Kiure, Msajili Msaidizi Kitengo cha Gharama za Uchaguzi na Elimu kwa Umma amesema kuwa hadi sasa vyama vitatu pekee ndivyo vilivyorejesha ripoti hiyo.

“Mwisho wa kurejesha ripoti ni kesho tarehe 25 na kwamba inagawa kesho siyo siku ya kazi lakini ofisi itakuwa wazi, hadi sasa vyama vitatu ndivyo vilivyorejesha, ambavyo ni CCM, ACT Wazalendo, na CUF,” amesema Kiure.

Kuhusu adhabu zilizoanishwa kisheria kwa vyama vinavyokutwa na hatia ya  kutorejesha ripoti hiyo, Kiure ameeleza kuwa zipo adhabu kwa chama au kwa wagombea.

“Sheria zinasema mgombea asiyefanya marejesho kuna adhabu zake endapo atapatikana na hatia, adhabu ni faini ya milioni miwili au kifungo cha mwaka mmoja na au vyote kwa pamoja,” amesema na kuongeza.

“Chama nacho kina adhabu ya faini isiyozidi milioni tatu, pamoja na faini hiyo hakitaruhusiwa kugombea kwenye uchaguzi unaofuata iwe mdogo au mkubwa mpaka itakapofanya marejesho na kwamba hakitagombea hadi kilete mrejesho,” amesema.

Aidha, Jaji Mutungi amevitaka vyama vya siasa kufuata utaratibu hali kadhalika ametoka wito kwa wanasiasa na wananchi kujenga mazoea ya kufanya utafiti na uchunguzi wa jambo lolote la kitaifa litakapotokea badala ya kutoa maamuzi ya haraka.

“Hatuwezi tukafanikiwa ikiwa hatuchambui vitu kwa upana na kuvitafakari kwa wakati hivyo basi ni lazima tujenge tabia ya kufanya utafiti na kudadavua mambo,” amesema na kuongeza.

“Tunasisitiza vyama vya siasa vifuate utaratibu. Na kama ndani ya chama kutatokea tatizo Wadau na wahusika kama hawajaleta barua ya malalamiko siwezi nikaingilia kati masuala yao kwa kuwa sheria inatutaka tusiingilie uendeshaji wa shughuli za chama.”

 

 

error: Content is protected !!