June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ofisa wa Serikali aficha mamilioni ‘hadi kwenye friji’

Spread the love

 

VITA dhidi ya dawa za kulevya imelipuka upya nchini Tanzania, baada kuanza kufahamika kwa mtandao wa watumishi ndani ya taasisi za umma, wanaoshirikiana na wafanyabiashara kufanya biashara hiyo haramu. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Katika vita hiyo, mtumishi wa taasisi moja ya Serikali, amekamatwa akihusishwa na dawa za kulevya, na kukutwa na mamilioni ya fedha akiwa amezisambaza chumbani mwake na kuzagaa karibu kila pembe.

Taarifa za ndani ya Serikali, zilieleza mtandao wa dawa za kulevya umelipuliwa na kufahamika, pamoja na kusuasua kwa wakuu wa baadhi ya taasisi kuchukua hatua, dhidi ya watumishi wao wanaotuhumiwa kuhusika na biashara hiyo.

Taarifa zilieleza, mmoja wa maofisa waliokamatwa, alikutwa na Sh.38 milioni na dola za Marekani 5,000 zimetapakaa chumbani anamoishi.

“Huyo alikutwa na fedha zimetapakaa chumbani mwake, zingine kwenye friji ndani na nje kwa juu.”

“Fedha zingine zikionekana kukaa muda mrefu hadi rubber bands (mipira ya kufungia fedha) zikiwa zimekatika kwa joto, na kukaa muda mrefu. Maana yake hakuwa anazihitaji,” alisema mtoa taarifa wetu jirani na anakoishi ofisa huyo.

Miongoni mwa wahusika, wamo katika taasisi zinazopaswa kudhibiti biashara hiyo, wakiwamo maofisa wa Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baadhi wakiwa tayari wamefikishwa mahakamani.

Wiki hii watumishi wawili wa TRA walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kufanya biashara ya mihadarati, wakiunganishwa na wafanyabiashara walioshirikiana nao, huku wengine wakiendelea kuchunguzwa.

Wakati watumishi hao wa TRA wakifikishwa mahakamani, maofisa wengine watano wa Polisi wanaendelea kuchunguzwa, watatu wakiwa wamekamatwa na mmoja akitarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote wiki hii.

Ofisa wa Polisi mwenye cheo cha Koplo (jina tunalihifadhi), amekutwa na sehemu ya dawa hizo, ambazo zinadaiwa kuibwa kwenye gari lililokamatwa na shehena ya dawa hizo Dar es Salaam.

Kukamatwa kwa ofisa huyo wa Polisi, kulisaidia kupatikana kwa maofisa wengine, ambao nao wanaendelea kufanyiwa uchunguzi, Gazeti la kila siku la Raia Mwema, lililoripoti habari hii, imebaini katika mfululizo wa uchunguzi wake.

“Kukamatwa kwa ofisa huyo wa Polisi, kumesaidia kuutambua mtandao mzima wa polisi wanaolinda wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Tayari orodha inafanyiwa kazi na wengine wamo katika hatua za mwisho kushtakiwa,” alieleza mtoa habari wetu serikalini.

Ofisa huyo wa Polisi, alikutwa ameuza sehemu ya dawa alizochota kwenye shehena iliyokamatwa, na kununua gari ambalo nalo lilikamatwa na kukutwa na kilo moja ya dawa za kulevya aina ya heroine.

Watumishi wa TRA waliofikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na dawa za kulevya ni pamoja na Andrew Paul (34), mkazi wa Kurasini, Dar es Salaam anayefanya kazi, Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Makao Makuu na mwenzake, Ally Juma Ally (32) mkazi wa Kinyerezi.

Paul ambaye ni ofisa wa kitengo cha usimamizi na ufuatiliaji wa kodi, makao makuu ya TRA, kitengo ambacho kinafuatilia na kudhibiti uhalifu wa kodi, alifikishwa mahakamani Jumatatu iliyopita na Ally alifikishwa mahakamani juzi Jumanne.

Watuhumiwa wengine waliofikishwa mahakamani walitajwa kuwa ni George Mwakang’ata (38) mkazi wa Mbagala Kuu, Temeke, Said Mgoha (45) wa Mtoni Kijichi, Temeke na Abubakar Juma (28) mkazi wa Kariakoo, Dar es Salaam.

Wote wanatuhumiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa jumla ya kilo moja na gramu 599.61, walizokutwa nazo katika mazingira tofauti, na wote wameshitakiwa kwa makosa yanayoangukia kwenye sheria ya uhujumu uchumi.

Hivi karibuni Raia Mwema iliandika kuhusu kuwapo watumishi kadhaa wa taasisi za umma, ikiwamo Polisi na taasisi zingine, wanaochunguzwa kwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.

Taarifa zinasema watuhumiwa zaidi wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni.

Washitakiwa hao ni sehemu ya watuhumiwa ambao wamekuwa wakichunguzwa na kuhojiwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Gerald Kusaya, aliiambia Raia Mwema juzi, kuwa kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa undani, hadi watakaponasa wahusika wote.

Hata hivyo, aligusia kwamba: “Vita dhidi ya wahusika wa mtandao wa dawa za kulevya ndiyo kwanza imeanza.”

Alisema watuhumiwa wakiwamo watumishi wa umma, watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na kukiri kuwapo watuhumiwa zaidi wanaotarajiwa kushitakiwa.

Hivi karubuni, washitakiwa wengine wawili, Abdallah Chande na Crispin Francis (Pina) walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Wawili hao, walishitakiwa kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine, zenye uzito wa kilo saba. Mashtaka mengine yanayomhusu Chrispin yalihusisha kukutwa na bangi.

Gazeti la Raia Mwema limekuwa likiandika kuhusu kuwapo kwa vigogo ndani ya Polisi, wanaotuhumiwa kusaidia mmoja wa wafanyabiashara nchini, kuficha sehemu ya ‘mzigo’ wa dawa hizo.

Hadi sasa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, kupitia kitengo chake cha upelelezi wa jinai, wanaendelea na uchunguzi wa kijinai dhidi ya maofisa wake, ambao hadi sasa baadhi walielezwa kuendelea kuwapo kazini na wengine kuwa mahabusu.

Miongoni mwa wanaotajwa kuhojiwa, ni pamoja na viongozi waandamizi wa Polisi, katika mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Mashitaka hayo dhidi ya usafirishaji wa dawa za kulevya, yanakuja wiki kadhaa, tangu Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya, kukamata gari likiwa na shehena ya dawa zenye uzito wa kilo 88.27, maeneo ya Kimara Korogwe, Dar es Salaam.

Dawa hizo aina ya heroin kilo 12.25 na methamphetamine kilo 76.2 zilikutwa kwenye viroba ndani ya gari hilo aina ya Toyota Prado.

Zilikamatwa baada ya kupatikana kwa taarifa ya kufuatiliwa nyendo za gari hilo, maeneo ya Magomeni.

Baada ya kulifuatilia kwa muda mrefu lilikutwa limetelekezwa Kimara Korogwe, na baada ya kufanyiwa uchunguzi, lilikutwa na dawa hizo, lakini dereva hakupatikana.

Aidha, kupatikana kwa taarifa hizo, kumekuja ndani ya kipindi cha siku 100 za utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia aliingia madarakani, Machi 19 mwaka huu, baada ya kufariki dunia kwa Rais John Magufuli.

Wakati wa kumwapisha Kusaya, Rais Samia alisema: “Nenda kakamate dawa za kulevya, tafsiri yake ni kubwa. Kuingia kwake ni tofauti. Sianga (William), alifanya kazi nzuri sana na Kaji (James) aliendeleza. Nenda ukafanye kazi. Nataka ukasimame kwenye kile kitengo. Pale una maisha ya vijana wetu.”

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Chrispin, anadaiwa kulindwa na kushirikiana na baadhi ya maofisa wa Polisi na taasisi zingine za Serikali, na kwamba baa yake ya Masaki, ilikuwa maarufu kwa biashara ya bangi na dawa za kulevya.

Mmoja wa maofisa anayetajwa kuficha kielelezo cha dawa za kulevya kutoka nyumbani kwa mtuhumiwa, alikana kufahamu lolote kuhusu madai hayo na kusema: “Mimi binafsi sijui chochote kuhusu hilo suala. Na pia mimi si msemaji wa Polisi.”

Hata hivyo, mmoja kati ya maofisa wa Polisi wanaotuhumiwa, anatajwa kuwa miongoni mwa maofisa waliopandishwa vyeo hivi karibuni, na sasa amehamishwa eneo la kazi mkoani Dar es Salaam.

error: Content is protected !!