October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Odinga akataa matokeo uchaguzi mkuu Kenya, kukimbilia mahakamani

Spread the love

 

ALIYEKUWA Mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa Kenya kupitia muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga leo Jumanne amekataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi huo na kubainisha kuwa atakwenda kuyapinga mahakamani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kenya … (endelea).

Matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na mipaka (IEBC), Wafula Chebukati, yalimpa ushindi naibu wa rais William Ruto kuwa ndiye rais Mteule.

Katika matokeo hayo Dk. Ruto kutoka chama cha United Democratic Alliance (UDA) alipata kura 7,176,141 dhidi ya kura 6,942,930 za mpinzani wake wa karibu, Raila Odinga wa muungano wa Azimio la Umoja.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Nairobi, Odinga amesema kwamba hakubaliani na matokeo hayo kwasababu mwenyekiti wa tume hiyo alikiuka katiba kabla ya kumtangaza mshindi

Amesema kwamba makamishna wa tume hiyo hawakukubaliana kuhusu hesabu ya mwisho ya matokeo hayo yaliompatia ushindi William Ruto.

”Takwimu zilizotangazwa na Chebukati ni batili kwa maoni yetu, hakuna mshindi kisheria, aliyetangazwa kihalali wala rais mteule’.

“Hatutakubali mtu mmoja ajaribu kuleta vurugu katika taifa letu na kubadilisha yale ambayo wakenya wameamua kama watu wamoja, wakenya hawatakubali na hatutakubali tutazidi kutetea watu wetu, katiba yetu katama wake ili Kenya kwenda mbele,” amesema Odinga.

Hata hivyo, Odinga amewataka wafuasi wake kudumisha amani na utulivu huku muungano huo ukifuata njia za kikatiba za kubatilisha matokeo ya Chebukati.

”Jana, demokrasia yetu changa ilikumbwa na msukosuko mkubwa, kwa sababu hiyo, Kenya inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisheria na kisiasa kutokana na matendo ya Wafula Chebukati.

”Tunafuatilia njia za kisheria na za amani. Tuna hakika kwamba haki itatendeka. Tunaelewa kuwa ni Chebukati pekee ndiye aliyejumlisha kura za urais. Aliwanyima makamishna wote kupata taarifa hizo”, aliongeza Raila akizungumza na vyombo vya habari jijini Nairobi.

error: Content is protected !!