June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ocean Road yaandaa matembezi kuikabili saratani ya matiti

Spread the love

TAASISI ya Saratani ya Ocean Road kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imeandaa matembezi ya hisani yenye lengo la kuhamasisha uchangiaji wa matibabu ya saratani ya matiti, anaandika Aisha Amran.

Julius Mwaiselage, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Ocean Road, amesema wamejitokeza ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kutokomeza saratani ya matiti na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu ugonjwa huo.

Akielezea kiundani juu ya matembezi hayo Mwaiselage amesema;

“Matembezi yanalenga kuchangia ununuzi wa vifaa vya kutolea tiba ya chemotherapy na wataendesha zoezi la uchunguzi wa saratani ya matiti. Ugonjwa huu ndiyo unaongoza duniani kwani kuna wagonjwa wapya 1.7 milioni wanaogundulika kila mwaka,” amesema.

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kwa mwaka 2012 zinaonyesha kila mwaka wagonjwa wapya 14.1 Milioni wamegunduliwa kuwa na ugonjwa huo na kati ya hao wagonjwa 8.2 Milioni wamefariki kwa ugonjwa huo.

“Kwa sasa vifo ni asilimia 13 ya vifo vyote ulimwenguni vitokanavyo na saratani na vinategemewa kuongezeka na kufikia 22 Milioni ifikapo 2030,” amesema Mwaiselage.

Aidha amesema katika mwaka 2015/2016, Taasisi hiyo ilihudumia wagonjwa 33,563 wakiwemo wagonjwa wapya wa saratani na wale wa marudio 20,297.

“Taasisi ilifanya uchunguzi wa saratani ya matiti na shingo ya kizazi kwa watu 7,134, ambapo kati yao 570 walikutwa na dalili za awali za saratani, na wanawake 84 walikutwa na saratani ya matiti huku 142 wakiwa na saratani ya shingo ya kizazi,” amesema.

Mgeni rasmi katika matembezi hayo anatarajiwa kuwa Dk. Hamisi Kingwangalla Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

error: Content is protected !!