December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

OCD kutoa ushahidi kesi ya Kigaila na wenzake

Spread the love

MASHAHIDI wapatao 10 akiwemo Mkuu wa kituo cha Polisi cha Kati, Dodoma Mjini (OCD), Deus Malingumu wanakusudia kutoa ushahidi katika kesi ya kufanya maandamano bila kibali inayowakabili makada wa Chadema pamoja na Mgombea ubunge jimbo hilo (Chadema), Benson Kigaila na wenzake 10. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Lina Magoma ulitoa kauli hiyo jana mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Fovo baada ya washtakiwa kutaka serikali kuthibitisha hoja walizozitoa.

Katika kesi hiyo yenye makosa matatu, Kigaila anakabiliwa na shitaka la lugha ya matusi kwa polisi huku Hadija Maura na Silvester Edmond wakidaiwa kumpiga askari polisi Rebeca kichwani kwa kutumia chupa ya soda aina ya fanta.

Akisoma maelezo ya awali, Lina alidai kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo Septemba 25 mjini hapa.

Alidai washtakiwa hao pamoja na wenzao ambao hawakukamatwa waliandamana bila kibali halali mara baada ya kumaliza mkutano wao stendi kuu ya mabasi kulekea stendi ndogo ya mabasi na walipoamriwa kutawanyika na maofisa polisi waliokuwa doria walikaidi amri hiyo.

“Hata hivyo walipoamriwa na polisi waliokuwa doria walikaidi, baada ya kukamatwa walifikishwa katika kituo cha kati cha polisi kwa ajili ya mahojiano na wakati wakiwa kwenye mahojiano alitokea Singo (Kigaila), ambaye alikimbia wasimkamate (kwenye maandamano), na kuongea matusi mbele ya OCD,” alidai Lina.

Hata hivyo, Wakili wa washtakiwa, Fred Kalonga alikubaliana na hoja kuwa washtakiwa walikamatwa, na kufikishwa mahakamani, majina, shughuli wanazojishughulisha nazo pamoja na anwani ya makazi yao.

“Tunakubaliana kuwa washtakiwa namba mbili hadi 11 waliwahi kukamatwa na kufishwa mahakamani lakini hatukubaliani na mazingira pamoja na mashitaka kwa hiyo tunataka serikali itudhibitishie,” amesema Kalonga.

Baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, Hakimu Mfawidhi Fovo, aliutaka upande wa mashtaka kuleta ushahidi wa hoja ambazo zinabishaniwa.

Washtakiwa wote wanaendelea na dhamana zao hadi Novemba 3 kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.

error: Content is protected !!