September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nyota ya Bernard Membe yazidi kung’aa

Spread the love

IKIWA imesalia miezi michache kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge wa madiwani wa Oktoba mwaka huu, nyota ya aliyepata kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC), kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe, inazidi kuimarika kisiasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Kujiimarisha kisiasa kwa Membe, kumeelezwa na baadhi ya wachambuzi, kuwa kunatokana na “uthubutu wake wa kusimama kuhesabiwa” na kueleza kile anachokiamini.

“Kila uchao, Membe anazidi kujiimarisha kisiasa, kutokana na uthubutu wake wa kusimamia kile anachokiami. Kuthibitisha haya angalia maandiko yake kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari kwa ujumla wake,” ameeleza mbunge mmoja wa Bunge la Jamhuri, ambaye hakupenda kutajwa gazetini.

Mbunge huyo ambaye anatokana na CCM amesema, katika siku za hivi karibuni, watu wengi wamekuwa wanamshabikia Membe, kutokana na kile anachokiita, “kuminywa kwa uhuru wa kujieleza nchini.”

Anasema, “Membe sasa ndio kama amebeba tumaini la wanyonge na tumaini la wasio na sauti, ambao katika utawala huu, wamekuwa wakitishwa mno na kusakamwa. 

“Kauli zake, zinafanana na sauti ya mtu aliaye Nyikani; na atengenezaye njia ya Bwana,” ameeleza mbunge huyo, kabla ya mwenzake wa upinzani kurukia na kusema, “Membe aweza kuwa Mussa mpya katika kizazi hiki.”

Alisema, maandiko matakatifu yameeleza kwa kirefu safari ya Mussa Mussa na watu wake ya kutoka Misri, kuvuka Mto Jodan hadi kufika nchi ya ahadi. 

Anasema, “lengo lao lilikuwa kufika nchi ya Kanaani. Lakini Musa hakufuata njia fupi zaidi, yaani umbali wa kilometa 400 hivi kupitia pwani yenye mchanga, njia ambayo ingewaelekeza moja kwa moja hadi Ufilisti, eneo la adui. Ndivyo Membe anavyovuka mabonde na milima hadi kuelekea Nchi ya Ahadi.” Hakufafanua.

Hata hivyo, waziri huyo wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa zamani wa Tanzania, akiandika katika ukurasa wake wa twitter, leo Ijumaa, tarehe 7 Februari 2020 anasema, “namshukuru Mungu kwa ujasiri alionipa wa kufika mbele ya kamati ya nidhamu” ya chama chake.

Jana Alhamisi, 6 Februari 2020, chama hicho tawala kilimhoji Membe na kikadai kuwa “makada wengine wawili waandamizi,” Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba, watahojiwa leo Ijumaa. 

Hadi sasa, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na CCM kuhusiana na kuhojiwa kwa viongozi hao. Kinana na Makamba, wamewahi kushika wazifa wa ukatibu mkuu wa chama hicho.

Desemba mwaka jana, katika kikao chake kilichofanyika jijini Mwanza, NEC iliagiza makada hao watatu kuhojiwa, kufuatia kuibuka kwa “minyukano ya ndani kwa ndani,” ya chama hicho.

Kinana, Makamba na Membe, “wanatuhumiwa kwa ukiukwaji wa maadili kwa mujibu wa katiba ya chama hicho na Kanuni ya Maadili na Uongozi.”

Taarifa iliyokuwa imetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, tarehe 13 Desemba 2019, ilieleza kuwa makada wengine watatu – Januari Makamba, Nape Nnauye na William Ngeleja – “wamesamehewa dhambi zao,” kufuatia hatua yao ya kumuomba radhi mwenyekiti wao, Rais John Pombe Magufuli.

Polepole alisema, wanachama hao waliomba radhi kwa Rais Magufuli, baada ya “kukiri mbele yake kufanya makosa ya kimaadili yaliyokidhalilisha chama na viongozi wake mbele ya umma.”

Wanachama hao watatu wa CCM pamoja na watatu ambao walitangazwa kuhojiwa jana – wote sauti zao – zilivujishwa kwenye mitandao, wakifanya mawasiliano kwa njia ya simu, wakizungumzia masuala mbalimbali kukihusu chama na mwenyekiti wake.

Sehemu ya mazungumzo yaliyovuja ya Mzee Yusuf Makamba na Kinana, ni pamoja na kuandaa taarifa ya malalamiko dhidi ya “mawanaharakati” Cyprian Musiba ambaye wanamtuhumu kwa “kuwadhalilisha,” bila kuchukuliwa hatua yoyote na kuhoji analindwa na nani.

Kwa upande Membe, licha ya sauti yake kusikika kwenye mazungumzo hayo yaliyovuja, amekuwa akituhumiwa na baadhi ya wanachama wenzake anajipanga “kumng’oa Rais  Magufuli’ katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Japo katiba ya CCM inaruhusu hilo, imekuwa ni ada ya chama kumuachia rais aliye madarakani kupita bila kupingwa kwa awamu ya pili ya urais wake.

Katika ujumbe wake aliyoutuma leo kwa umma, Membe ameeleza kuwa bado yeye “yuko imara na hata yumbishwa.”

Alisema, “nimerejea Dar es Salaam salama, kutokea Dodoma. Namshukuru Mungu kwa ujasiri alionipa wa kwenda mbele Kamati  ya Maadili na nidhamu na kujibu hoja mbalimbali bila woga, bila kuyumba na wala kuyumbishwa!”

Aliongeza: “Naamini wameupokea ushauri niliyoutoa kuhusu Uhuru, Haki, Uchaguzi na uhusiano wa kimataifa….”

Bernard Kamilius Membe (66), alizaliwa katika eneo la Rondo, Chiponda, mkoani Lindi, akiwa ni mtoto wa pili kati wa watoto saba (7) wa Mzee Kamillius Anthony Ntachile na Mama Cecilia John Membe. 

Membe ambaye alipata mafunzo ya ukachero na baadaye kuajiriwa kwenye Idara ya Usalama wa taifa (TISS), alipata shahada yake ya pili nchini Marekani, katika chuo kikuu cha kimataifa cha Johns Hopkins. Alijikita katika masuala ya upatanishi, mahusiano ya kimataifa na sheria zake. 

Alikuwa nguzo muhimu ya mahusiano ya kimataifa kati ya serkkali ya Tanzania na mataifa mengine ulimwenguni, wakati akihudumu kama waziri wa masuala ya kigeni, katika serikali ya Rais Jayaka Mrisho Kikwete.

Membe alikuwa wa kwanza kufika kwa mahojiano hayo Alhamisi asubuhi, na kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Philiph Mangula, baada ya kukamilika kwa mahojiano kati ya Membe na kamati yake, atafuatia Kinana na kisha Makamba. Kila mmoja anatarajiwa kuhojiwa kwa siku moja.

Amesema, “tumepanga kuwahoji kwa siku moja kila mmoja, lakini utaratibu unaweza kubadilika kulingana na maelezo atakayotoa mhusika. Kama tutaona siku moja haitoshi, atarejea tena siku inayofuatia.” 

Kwa mujibu wa Mangula baada ya kuhitimisha kazi yao, vikao vya chama vitapitia maelezo ya watuhumiwa hao na kutoa maamuzi.

Baada ya mahojiano ya saa tano Membe amewaambia waandishi wa habari kuwa alikuwa na mkutano mzuri.

Alisema, “nimepata nafasi nzuri ya kufafanua mambo kadhaa ambayo chama changu ilitaka kuyajua…Safari hii ya kuja Dodoma imekuwa na manufaa makubwa sana, sana kwangu, kwa chama na kwa taifa letu…mengine yatakuwa yanapatikana kidogo kidogo nikishiba.”

Swali ambalo baadhi ya wachambuzi wanajiuliza: Ni adhabu gani wanayoweza kupatiwa makada hao waandamizi endapo watakutwa na hatia?

Kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM, Toleo la 2017, zimetajwa adhabu tatu kwa wanachama wanaofika mbele ya kamati hiyo.

Kwamba, kifungu cha 5(2) kinasema; wanachama wanaovunja maadili ya chama kama yalivyoainishwa katika katiba ya CCM na kanuni za CCM wanachukuliwa hatua za kuwarekebisha na kama itashindikana kuwarekebisha ni kuwaondoa katika chama au katika uongozi.

error: Content is protected !!