Friday , 19 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Nyongeza kahawa ya Karagwe ni TZS 106/= kwa kilo
Habari Mchanganyiko

Nyongeza kahawa ya Karagwe ni TZS 106/= kwa kilo

Innocent Bashungwa, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo
Spread the love

CHAMA cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa Karagwe na Kyerwa (KDCU) kinadaiwa kuwatangazia wakulima kwamba watapata malipo ya nyongeza mwezi huu wa Januari 2019, ambapo ngongeza ni kiasi cha TZS 106/= kwa kilo. Anaripoti Deusdedith Kahangwa, Karagwe … (endelea).

Kupitia tangazo la tarehe 07 Juni 2018, lenye kumbukumbu namba KDCU/RPCC/25/IX/82, na lililosainiwa na Kaimu Meneja Mkuu wa KDCU wa wakati huo, Kakulu B. Kakulu, KDCU walitangaza kwamba, “bei ya awali ya kilo moja ya kahawa ya maganda kwa kahawa zote za Arabika na Robusta ni kiasi cha TZS 1,000/=.”

Tangazo hilo lilifafanua kwamba, “malipo ya pili yatapatikana baada ya kahawa kuuzwa mnadani.” Kiwango cha malipo ya pili hakitajwi katika tangazo hilo. Sasa imefahamika kwamba nyongeza iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu ni TZS 106/= kwa kilo.

Wakiongea na wandishi wa habari hii, wakulima kadhaa kutoka Karagwe na Kyerwa walieleza kushtushwa na kiwango cha bei ya nyongeza kilichotangazwa na KDCU. Mshtuko wao unatokana na ukweli kwamba, katika msimu wa mwaka jana, yaani 2016/17, bei ya kahawa ilikuwa TZS 2,000/= kwa kilo.

Mkulima mmoja amelalamika kwamba, kwa kuzingatia kuwa nyongeza iliyotangazwa na KDCU ni wazi kwamba, bei imeporomoka kwa 45%. Anaeleza kwamba, kwa vile mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa Karagwe ni 80%, ni wazi kwamba, umaskini wa Karagwe umeongezeka mara mbili.

Mkulimamwingine kutoka Kyerwa alieleza kushangazwa kwake na ukweli kuwa, pamoja na jitihada za serikali za kuondoa wanunuzi wa kati, bado bei ya kahawa imezidi kushuka badala ya kupanda.

Kaimu Meneja wa KDCU, Oscar Dominick, alipopigiwa simu ili athibitishe taarifa hizi hakupokea. Hata ujumbe mfupi wa maandishi haukujibiwa. Mwandishi wa habari hii alimtumia ujumbe ufuatao: “Meneja, nimepata habari kuwa wakulima wa kahawa Kargwe watapata malipo ya nyongeza hivi karibuni. Ni kiasi gani kwa kilo na watalipwa lini?” Ujumbe huo ulitumwa saa 7.44 mchana wa 02 Januari 2019.

KDCU ni chama cha Msingi kinachohudumia wakulima wa kahawa katika wilaya za Karagwe na Kyerwa tangu 1990. Kinaripotiwa kuwa na wanachama 4,000 kati ya wakulima wa kahawa wapatao 64,000. Kina vyma vya msingi 96. Kwa sasa, Mwenyekiti wa KDCU ni Anselin Kabateraine.

Kwa mujibu wa Mkakati wa Maendeleo wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) wa 2011/21, Dira ya bodi ni: “Kuwajengea wadau wote tasnia ya kahawa endelevu yenye kuleta faida na ya muda mrefu, inayozalisha kahawa ya Arabika na Robusta ya ubora wa hali ya juu inayokubalika kimataifa na kutoa mchango muhimu kwa uthabiti wa uchumi mkubwa, upunguzaji wa umaskini na uboreshaji wa riziki ya watanzania.”

Na dhima ya Tasnia ya Kahawa Tanzania ni, “Kuongeza uzalishaji na ubora wa kahawa kitaifa ili kuboresha mapato katika mnyororo wote wa thamani, hususan wakulima wa kahawa.”

Kwa mujibu wa utafiti wa Winnie Nguni na Henry Chalu (2014), wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, minyororo ya hatua za kuonngeza thamani ya kahawa nchini Tanzania inahusisha wadau tisa.

Kuna soko la pembejeo, wakulima, makampuni ya kuendeleza wakulima (estates), ushirika wa vikundi vya wakulima (FGAs), vyama vya msingi vilivyoko vijijini, wanunuzi binafsi wa kahawa (PCBs), vyama vya ushirika ngazi za wilaya, soko la mnada Moshi linaloendeshwa na Bodi ya Kahawa Tanzania, na Soko la Kimataifa linalohusisha wanunuzi walioko katika mabara mbalimbali.

Kwa kuzingatia idadi ya wadau wanaoshirikiana katika mnyororo husika, kuna njia kuu sita zinazofahamika, ambapo njia yoyote kati ya hizo sita, inaweza kumuunganisha mkulima wa kahawa na soko la kimataifa (tazama mchoro hapa chini).

Njia ya kwanza ni mnyororo wenye hatua zifuatazo: wakulima, wanunuzi binafsi, soko la mdana Moshi, na Soko la Kimataifa. Njia ya pili ni mnyororo wenye hatua zifuatazo: wakulima, wanunuzi binafsi, na Soko la Kimataifa.

Njia ya tatu ni mnyororo wenye hatua zifuatazo: wakulima, vyama vya msingi, chama cha ushirika, soko la mnada, na soko la kimataifa. Njia ya nne ni mnyororo wenye hatua zifuatazo: wakulima, ushirika wa vikundi vya wakulima, soko la mnada Moshi, na soko la Kimataifa.

Njia ya tano ni mnyororo wenye hatua zifuatazo: wakulima,makampuni ya kuendelelza wakulima (estates), soko la mnada Moshi, na Soko la Kimataifa. Na njia ya sita ni mnyororo wenye hatua zifuatazo: wakulima, makampuni ya kuendelelza wakulima (estates), na Soko la Kimataifa.

Mkulima anaweza kupata bei nzuri kwa sababu tatu kubwa. Kwanza, ni kutokana na upatikanaji wa bei nzuri ya kahawa katika soko la dunia. Takwimu zinaonyesha kwamba, baada ya mafuta, kahawa ni zao la pili kununuliwa sana kwenye soko la dunia. Aidha, kahawa ni kinywaji cha tatu duniani, baada ya maji na soda. Kwa sababu hizi mbili, bei ya kahawa katika soko la dunia haijawahi kushuka kwa zaidi ya asiliamia 50%

Pili, ni ni kutokana na ufupi wa mnnyororo wa hatua za kuongeza thamani ya zao la kahawa. Mnyororo mrefu unamaanisha bei ndogo, na mnyororo mfupi unamaanisha bei kubwa, kwani wanunuzi na wachuuzi wa kati wanamega fedha ya kahawa.

Na tatu mkulima anaweza kupata bei nzuri kama kuna uwazi na mawasiliano ya karibu kati ya wadau walio katika mnyororo husika wa kuongeza thamani ya kahawa. Kama mawasiliano ni hafifu na hakuna uwazi, hata kama kuna bei nzuri katika soko la dunia, mkulima atanyonywa tu.

Kama mchoro unavyoonyesha hapo juu, utafiti wa Winnie Nguni na Henry Chalu (2014), kulikuwa na mawasiliano duni kati ya mkulima, vyama vya msingi, vyana vya ushirika na Bodi ya Kahawa inayoendesha mnada wa kahawa Moshi.

Malipo ya nyongeza ya Shs. 106/= kwa kilo, kama ilivyotolewa kimya kimya kwa wakulima wa kahawa Karagwe, ni ushahidi tosha kwamba, tatizo hili bado lipo hata leo 2019.

“Waziri wa Kilimo, Bodi ya Kahawa Tanzania na Uongozi wa KDCU Ltd wanapaswa kuwaeleza wakulima wa Kahawa Karagwe kilichotokea mpaka bei ya kahawa ikaporomoka kwa asilimia 45,” alisema mdau mmoja aliye mzoefu katika tasnia ya kahawa kwa muda mrefu, lakini asiyependea kutajwa jina lake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

Habari Mchanganyiko

Mume auwa mke kwa kumchoma visu, ajisalimisha Polisi

Spread the loveJACKSON Kalamji (49), anashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Mwanza,...

error: Content is protected !!