January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nyerere hajaenziwa, tusidanganye

Mwalimu Nyerere

Image 2

Spread the love

JUMATATU ya 14 Oktoba 2013, taifa liliadhimisha miaka 14 ya kifo cha mwasisi wake, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Sherehe za maadhimisho zilifanyika mkoani Iringa.

Mwalimu Nyerere alifariki dunia 14 Oktoba 1999 kwenye hospitali ya St. Thomas jijini London, Uingereza. Alikuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa saratani ya damu (leukemia).

Akihutubia taifa kutoka mkoani Iringa, ambako sherehe za maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu zilifanyika, Rais Jakaya Kikwete alisema, “…taifa bado ni wamoja. Tusikubali kugawanywa kwa misingi ya tofauti za rangi, dini, itikadi au rasilimali.”

Alisema Mwalimu Nyerere alilijenga taifa kwenye misingi ya umoja; yeye na serikali yake watahakikisha umoja wa kitaifa unaendelea kudumu.

Hata hivyo, kinyume na maelezo ya rais kuwa bado taifa tuko wamoja; ukiangalia yanayojiri ndani ya serikali yake, chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jamii kwa jumla, huhitaji kuleta mtafiti kutoka nje, kubaini taifa hili tayari limezama katika migawanyiko.

Taifa limegawanyika kidini, kisiasa, kijamii, kirasilimali, kiitikadi na hata kiutu. Ni tofauti na wakati wa Nyerere. Yeye alitetea maslahi ya taifa lake na watu wake, bila ubaguzi. Aliheshimu haki ya kila raia.

Nyerere alifanya hivyo kwa sababu, alitanguliza maslahi ya taifa kwanza kabla ya chama chake na familia yake. Leo hii, miaka 14 baada ya Nyerere kuondoka duniani, raia wa Jamhuri ya Muungano wanapigwa kama wanyama na hakuna hatua zinazochukuliwa. Ni kwa sababu watawala wameligawa taifa kwenye matabaka la walionacho na wasionacho.

Ni tofauti kabisa na wakati wa Mwalimu Nyerere ambapo mtoto wa maskini hakuwa na tofauti na mtoto wa tajiri au kiongozi. Watoto wa Nyerere waliishi maisha ya kawaida. Walisoma kwenye shule za kawaida karibu sawa na hizi zinaitwa leo “shule za kata.” Walisoma kwenye vyuo vilevile.

Kwenye vyombo vya sheria walihudumiwa kama raia wengine. Ni tofauti na sasa. Viongozi wengi wanasomesha watoto wao kwenye shule za kimataifa.

Hivi ndivyo Nyerere alivyolijenga taifa lake. Wakati wake, raia wote walikuwa na haki sawa. Lakini sasa kwa kuwa tumeacha misingi aliyotuachia, ndiyo maana watu kama Dk. Steven Ulimboka, wanapigwa, wanatekwa na wanateswa hadi kuwa nusu mfu.

Naye Absalom Kibanda amepigwa kama mnyama. Lakini hakuna aliyekamatwa. Daudi Mwangosi amepigwa bomu huku Michael Kamuanda, kamanda wa polisi mkoa wa Iringa akishuhudia. Hakuhojiwa wala kuwajibishwa. Ni tofauti na ilivyokuwa enzi za Nyerere.

Wakati wa utawala wake na hata baada ya kustaafu urais, Nyerere  alisimamia utumishi wa umma ili uonekane kuwa ni wito. Hivi sasa, utumishi wa umma ni miradi ya kujitajirisha. Ni mradi wa kukomoa wengine.

Nyerere alipinga uwekezaji na uuzaji wa mashirika ya umma. Ubinafishaji kwenye migodi. Bandari, viwanda na mashamba yakiwamo ya mkonge na tumbaku. Aliita uwekezaji huu, ni wizi wa mchana.

Leo, miaka 14 baada ya Nyerere kuondoka, karibu kila rasilimali ya taifa hili inauzwa au kukodishwa kwa wageni.

Miaka 14 bila Nyerere, ni vigumu kumtaja kiongozi mwadilifu ambaye kama angekuwa hai, angesema “huyu hapa msafi.” Hata Benjamin Mkapa, rais mstaafu aliyepigiwa chapuo na Nyerere hadi kuitwa, “Mr. Clean” hawezi tena kuitwa jina hilo.

Utawala wa Mkapa ndio ulioruhusu na kusimamia uuzwaji – kwa bei ya bure – Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), kiwanda cha viatu cha taifa (BORA), Shirika la Bima la Taifa (NIC), shirika la ndege la taifa (ATC), wizi wa fedha za umma kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT), uwekezaji kwenye bandari, migodi, mashamba na viwanda.

Mkapa ndiye aliyevunja misingi ya uadilifu hadi kusababisha baadhi ya viongozi kushiriki kwenye wizi wa mali ya umma, uuzaji wa dawa za kulevya, ujangili wa wanyamapori, uongo, ghiliba na mengineyo.

Baadhi yao wanatumia nafasi walizokabidhiwa kujilimbikizia mali ili kuweza kuishi vizuri wao na familia zao, huku raia waliowengi wakitopea kwenye umaskini.

Wanahudumiwa tofauti kwenye vyombo vya dola – mahakama, polisi na hata magereza.

Ndani ya CCM, tofauti na wakati wa Nyerere, uongozi unalanguliwa kama bidhaa sokoni. Bila rushwa, hila, ghiliba, huwezi kupata uongozi.

Chaguzi nyingi kuanzia zile za chama hadi serikali, zimegeuka miradi ya matajiri, tena inayogharimu mabilioni ya shilingi. Hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa na watawala kukomesha jambo hili. Wanashindwa kwa sababu, wengi wao wamepatikana kwa njia za rushwa.

Mifano ni mingi. Jimboni Bariadi Magharibi, mgombea mmoja wa ubunge alituhumiwa kugawa rushwa ya fedha, chumvi, sukari, kanga, vitenge, mabati, baiskeli na hata pikipiki. Hakuna aliyemuuliza.

Katika mazingira haya, hakuna anayeweza kusema taifa ni moja, wala hakuna anayeweza kusimama na kudai taifa hili bado linamuenzi Nyerere. Anayesema hivyo atakuwa anajifurahisha tu.

error: Content is protected !!