January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nyerere alijua CCM itaanguka

Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM

Spread the love

KIMSINGI Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alishakichukia Chama Cha Mapinduzi (CCM) miaka michache kabla ya kifo chake, japo hakupenda kianguke akingali hai. 

Nyerere aliposema bila CCM imara Tanzania itayumba, hakumaanisha CCM itawale milele bali kama chama tawala kwa wakati huo wasipokuwa imara imara katika usimamizi wa utawala bora, taifa litayumba.

Maana yake ni kwamba, chama chochote kinapokuwa ndani ya utawala lazima kiwajibike kusimamia vyema rasilimali za taifa kwa manufaa ya umma, kinyume chake wananchi hukichukia hata kabla ya uchaguzi.

Mwalimu Nyerere alisema hivyo akijua namna nzuri ya kuondoa chama madarakani ni uchaguzi. Lakini alijua pia kuwa chama kikikosa uimara kabla ya uchaguzi baada ya hapo nchi itayumba.

Uimara wa chama aliolenga Nyerere ni ule wa kusimamia haki, katiba na sheria za nchi.

Kwa mfano, chama kinachowaogopa mafisadi si chama imara. Chama kinachowapendelea matajiri na kuwapuuza masikini si imara na hata kila kisichozingatia utawala wa sheria nacho si imara.

Nchi inayotawaliwa na chama legelege ni sawa na basi linaloendeshwa na dreva anayesinzia sinzia.

Uimara wa chama katika kusimamia sheria za nchi si sababu ya kutawala milele kwa kuwa nchi inahitaji sera bora na utawala wa sheria kwa pamoja.

Ili nchi iendelee ni lazima mawazo mbadala yaheshimiwe. Leo hii utawala wa sheria CCM wameshindwa, sera zao zimeshindwa kuboresha maisha ya Mtanzania.

Sasa tumaini pekee lililobaki kwa Watanzania ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) chini ya vyama makini vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Nyerere asingeweza kuwa mjinga kiasi hicho cha kuamini eti CCM inapaswa kutawala milele. Ndio maana akasema “Watanzania wakiyakosa matarajio yao ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM.”

Mwandishi wa makala haya ni Eliasanti Bugenyi ambaye anapatikana kwa barua pepe; ellybugenyi@yahoo.com

error: Content is protected !!