October 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Nyaronyo umetoka wapi na Lowassa?

Edward Lowassa, aliyekuwa Mgombea Urais kwa tiketi ya Ukawa

Spread the love

NIMESOMA makala mbili mfululizo za Nyaronyo Mwita Kicheere, zinazomjadili Edward Ngoyai Lowasssa, waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya mkataba tata wa kufua umeme wa Richmond.

Makala hizi zimeandikwa kwa dhana moja tu – kumsafisha Lowassa. Basi!

Lakini hebu tujiulize maswali yafuatayo: Kwa nini Kicheere ameamua kumsafisha Lowassa? Nani amemtuma? Amefanikiwa kumuondoa Lowassa katika lindi la tuhuma za ufisadi? Je, kipi kifanyike katika kipindi hiki kwa waandishi wa habari na makala wenye uwezo mkubwa aina ya Kichere?

Kwa hisia zangu, ambazo naamini ni za kweli, kuna mtu au kikundi cha watu wameona uwezo mkubwa wa Kicheere katika kuandika, wakamuomba au wakamshawishi  afanye kazi hii kubwa ya kumsafisha Lowassa.

Lakini badala ya Kicheere kumsafisha Lowassa, amemwingiza kwenye tope. Makala zake zote hazikujadili kwa mapana, utajiri wa Lowassa na jinsi alivyoupata.

Kicheere anasema Lowassa amepata utajiri wake kwa sababu alifanya kazi ya udalali wa viwanja Jijini Arusha. Anadai kuwa Lowassa alipata utajiri wake baada ya kuuza shamba katika eneo la Njiro. Ni vema akamtafua Lowassa ili amueleza jinsi alivyojipatia utajiri wake – kama ni kweli ni tajiri mkubwa hapa nchini – kuliko kutaka kupotosha ukweli.

Miaka ile ya utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi ambayo ndiyo inayotajwa na Nyaronyo kuwa Lowassa alikuwa dalali wa viwanja, ardhi ilikuwa bado inatawaliwa na sheria ya Ardhi Sura Na. 113 ya 1923 (The Land Ordinance Cap.113).

Kama eneo la Njiro lilikuwa shamba, ilibidi litumike kama shamba. Si vinginevyo. Kama halmashauri ya manispaa ya wilaya iliona eneo linahitajika kwa matumizi mengine, kama makazi, viwanda au huduma zingine za umma, serikali ingelitangaza hivyo kupitia vikao vya halmashauri husika.

Kama hakuna pingamizi baada ya siku 90, serikali inatwaa eneo hilo kwa kutumia Sheria Na. 47 ya mwaka 1967 iitwayo sheria ya kutwaa ardhi – The Land Aquization Act Na. 47of 1967.

Baada ya mmiliki wa awali kulipwa fidia kamili, halali na kwa wakati, ndipo serikali inaingia kwenye eneo husika na kulipima kulingana na michoro ya mipango miji na viwanja vinavyopatikana.

Kwa wakati huo, ilikuwaje Lowassa apimiwe eneo la shamba lake lote, halafu yeye ndiye auze viwanja vilivyotokana na eneo la shamba? Alitumia sheria ipi, kanuni zipi na taratibu zipi? Gharama za kupima viwanja vyake alilipia wapi? Alitumia kiasi gani?

Majibu ya maswali haya ni muhimu ili kuzuia ghiliba zinazoandaliwa na baadhi ya watu waliojipa kazi ya kumsafisha Lowassa.

Nijuavyo mimi, Lowasa aliwahi kufanya kazi sehemu mbalimbali nchini. Alianzia huko Tanu Youth League, baadaye Arusha International Conference Center (AICC), na baadaye akawa waziri katika ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia majanga na maafa.

Katika kipindi hicho, ndipo serikali ilipoamua kuagiza magari ya kifahari aina ya Pajero na Land Cruser (mashangingu) kutoka Japan, badala ya magari ya kawaida yaliyokuwa yamezoeleka ya LAND LOVER 109 na baadaye Tid 110 yaliyotengenezwa nchini Uingereza.

Land Rover yalikuwa ya bei ndogo kabisa lakini magari imara sana hasa kwa barabara zilizopo nchini. Baadaye akafanywa kuwa waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya mijini.

Alipokuwa Waziri wa Ardhi alifanya kazi kubwa lakini alijulikana kama mzee wa 50%. Inahisiwa huko ndiko Lowasa alipoibuka na utajiri. Ni vema ndugu yetu Nyaronyo Kicheere akaangalia sehemu hizo.

Yukimkini Kicheere na wenzake wanaotaka kumsafisha Lowassa wameshindwa. Wameendelea kumtumbukiza kwenye matope.

Hii ni kwa sababu, mbali na madai ya utajiri usioweza kuelezeka jinsi ulivyopatikana, Lowassa hawezi kujisafisha mbele ya jamii, juu ya matumizi mabaya ya madaraka na hasa  kuhusu alivyoingiza kampuni ya Richmond nchini.

Maelekezo yote kuhusiana na utoaji mkataba kwa Richmond yalikuwa yakifanyika chini ya Lowassa. Hii ni kwa mujibu wa waziri wa nishati wakati huo, Dk. Ibrahim Msabaha.

Ilibainika katika kikao baina ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za serikali na makatibu wakuu wa Fedha na Nishati, kwamba TANESCO ililazimishwa na serikali kuingia mkataba na kampuni hiyo.

Kwa maelekezo ya Lowassa, serikali ilitupilia mbali sheria zote za manunuzi na mikataba ili “kulazimisha na kulinda Richmond kupewa zabuni.”

Kamati teule ya bunge, katika uchunguzi wake wa kashfa hii, pamoja na kutaja wahusika wote na kutaka wawajibishwe, ilimwacha waziri mkuu “kuchukua uamuzi” anaoona unafaa. Lowassa alijiuzulu.

Taarifa zinaonyesha serikali iliingia mchakato wa kupata mzabuni, hata baada ya TANESCO kuona kuwa hakukuwepo mshindi kwa mujibu wa zabuni.

Kinyume cha maoni ya TANESCO, wizara ya nishati, baada ya kupitia maombi ya zabuni, iliamuru bodi kukubali kuwa Richmond ndiye mshindi, na 19 Juni  2006 wizara ikaagiza TANESCO kusaini mkataba na Richmond.

Katika uchunguzi wa bunge, ilibainika kuwa Richmond haikuwa na fedha, uwezo wa kiufundi, vitendea kazi wala uzoefu katika miradi kama hii.

Kwa mujibu wa Ibara ya 68 ya sheria ya manunuzi ya mwaka 2004, jukumu la kuamua mshindi wa zabuni ni la bodi ya zabuni ya shirika (TANESCO).

Mkataba wa Richmond ulirithiwa na kampuni ya Dowans Holdings SA ya Costa Rica na Dowans Tanzania Limited (DTL), ambayo nayo ikauza mkataba wake kwa Symbion Power, inayoendelea kuangamiza uchumi wa taifa.

Kwa msingi huo, Nyaronyo hajafanikiwa kutushawishi kumuamini Lowassa kuwa ni mtu safi. Mwadilifu na mchapa kazi.

Mwandishi wa makala hii, Crispina Kiemi amejitambulisha kuwa msomaji wa gazeti hili. Anapatikana kwa emeili:postyankar@yahoo.com

error: Content is protected !!