January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nyalandu: Tutawekeza kwanza kwenye rasilimali watu

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akiingia uwanjani tayari kwa kutangaza nia

Spread the love

LAZARO Nyalandu (44), Waziri wa Mali Asili na Utalii, emetangaza nia ya kuingia katika mbio za kuomba uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili apitishwe kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, na kuainisha kwamba ikichaguliwa, Serikali yake kwanza itajielekeza kuwekeza katika rasilimali watu. Anaandika Edson Kamukara, Singida … (endelea).

Nyalandu ametangaza nia leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Namfua mjini Singida, huku akitumia muda mwingi kuelezea mafanikio yaliyopatika katika wizara yake, na hivyo kumshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kumwamini na kuteua kuwa miongoni mwa mawaziri wake.

Tofauti na watangaza nia wengi ambao wamekuwa wakipigana vijembe na kuikosoa serikali ya Rais Kikwete, Nyalandu amewasifu marais wote wanne akisema wameifanikisha Tanzania kupiga hatua ya maendeleo, na kuwahadharisha wenzake akisema “tunaochukua fomu katika kinyangang’anyiro hiki naomba ndimi zetu zitawaliwe na hekima na busara. Tuwaheshimu wazee wetu waliotangulia.”

Nyalandu ambaye alihutubia kwa dakika 32, amesema anakusudia kuchukua fomu mjini Dodoma kesho, huku akisisitiza kwamba wamejitokeza wengi lakini baada ya ushindani apatitishwa mwana CCM mmoja wa kupeperusha bendera.

Amesema “Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi sana! Milima, mabonde, maziwa, misitu, madini, gesi, lakini rasilimali watu ndio muhimu na ni kubwa kuliko zote.”

“Katika hatua ninazozianza leo, tutapaswa kama Taifa kuongeza nguvu na kuhakikisha kila mtanzania anafanikiwa kwa kufanya jitihada za makusudi kuwekeza katika jamii, hii ikiwa na maana ya kuipa jamii ya Watanzania nguvu na uwezo wa kushiriki katika shughuli za kujiletea maendeleo.

“Kama nchi, tutapaswa kuongeza msukumo mpya wa kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia sekta zote muhimu zikiwapo kilimo, biashara, utalii, madini,”amesema.

Nyalandu amefafanua kuwa, uwezeshaji wa jamii kiuchumi utajenga ajira endelevu: “Tunataka jamii yenye maono, ujasiri, upendo, umoja na makusudi yenye dhamira ya maendeleo kwa wote.”

Ameongeza “naamini katika ushirikishwaji wa wananchi, kwani kufanikiwa kwa nchi yetu, kutategemea ni kiasi gani tunawajengea wananchi uwezo na kukata mizizi ya matatizo.”

Kwa mujibu wa Nyalandu, hatua hii italiwezesha taifa kumudu changamoto zitokanazo na matatizo au migogoro katikati ya wana jamii. Itakuwa muhimu kupiga vita ubaguzi wa aina zote, chuki, hila, woga, uonevu, ukatili, unyanyasaji, na dhuluma ya aina yeyote katika uotoaji wa huduma kwa wananchi.

“Hatua zangu nitazikanyaga kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa kwa wote, kwani imeandikwa, haki huinua Taifa.”

Nyalandu ambaye ameongoza Jimbo la Singida Kaskazini kwa vipindi vitatu vya miaka 15 kuanzia mwaka 2000, amesema chini ya uongozi wa  Rais Kikwete, kama waziri wa Mali Asili na Utalii ambayo sasa inaongoza katika kulipatia Taifa fedha za kigeni.

“Pia inachangia zaidi ya robo ya pato lote la Taifa, na kutoa ajira za moja kwa moja laki tano, huku Watanzania zaidi ya milioni mbili wakinufaika na biashara ya utalii nchi,”amesema.

Ameongeza kuwa katika hatua ya kupokezana kijiti kupitia CCM, na kama inavyoainishwa katika Ilani ya uchaguzi ya chama 2010-2015, “nitawatazama vijana wa nchi yetu kuwa ni sekta kamili.”

Nyalandu amesema “vijana sio tu kwamba ni shauku ya Taifa, mimi naamini kuwa vijana wa Tanzania sio mizigo wala sio bomu linalosubiri kulipuka.

“Vijana ni hazina, na vijana ni sekta muhimu sana kwenye maendeleo ya taifa letu. Hatuna budi kumuwezesha kijana wa Kitanzania ili awe nguvu kazi ya taifa letu. Tuwape vijana nafasi ya kuleta maendeleo chanya! Vijana wana hamu na shauku ya kuchangia katika maendeleo ya taifa.” 

Amesema kuwa anapochukua hatua hizi, na kuelekeza macho yake ulingoni ili kukiomba chama chake kimpe fursa ya kukipokea kijiti hiki, “nawaona vijana wa Tanzania kuwa ni fursa.”

Amesema “kwa kuangalia vijana kama sekta itatulazimu tuwe na mikakati endelevu, ya kumjengea uwezo kijana kuanzia kwenye elimu, na kumfanya akimaliza shule ya msingi au kidato cha nne awe na uwezo wa kujiajiri na kuajiri.

“Naona umuhimu na ulazima kwa vijana wa kitanzania kushika usukani wa maendeleo na mipango thabiti itawekwe kufanikisha azma kwenye kila sekta.”

 Kuhusu ardhi, amesema “katika kumuwezesha mtanzania, lazima suala la umiliki wa ardhi lifanikishwe. Ardhi ni jambo nyeti na linaenda sambamba na uzalishaji.

“Ardhi ni muhimu kwa kilimo na pia ni mali inayowezesha mtu kuzalisha na kupata faida mbali mbali. Umiliki wa ardhi unamfanya mtu akasikilizwa, akaaminiwa na akakopesheka.”   

Kwamba, hatua hizi zinaendelea kumhakikishia Mtanzania kupata elimu inayomuwezesha kujiajiri na kuajiriwa, na kwa kuboresha zaidi sera ya umiliki wa ardhi, watamjengea mtanzania uwezo mpya kiuchumi.

Sekta isiyo rasmi, Nyalandu amesema ili kujikwamua kiuchuumi inabidi sekta isiyo rasmi isiogope kuwa sekta rasmi. “Na sisi serikali tuondoe vikwazo vinavyojenga hiyo hofu.”

Pia amegusia bidhaa imara kwa bei ya ushindani, wakulima na wafugaji, utalii na usalama.

error: Content is protected !!