July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nyalandu, Nyalali, Mulenda wachukua fomu

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akiwa na mkewe Faraja Nyalandu

Spread the love

LAZARO Nyalandu, aliye Waziri wa Maliasili na Utalii, amekuwa miongoni mwa makada watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliokabidhiwa fomu za kuomba uteuzi wa kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Anaandika Edson Kamukara, Dodoma … (endelea)

Makada wengine ni Peter Nyalali, aliye mtoto wa Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, hayati Francis Nyalali na Leonce Mulenda, aliye Mkurugenzi wa Kampuni ya High Quality Consultancy Limited (HQCL), na hivyo kufanya idadi ya makada walichuoa fomu hadi leo mchana kufikia 16.

Nyalandu ndiye alikuwa wa kwanza kuchukua fomu katika Makao Makuu ya CCM Dodoma saa 5:00 na kasha kuzungumza na waandishi wa habari pamoja na wafuasi wake waliojitokeza kumsindikiza, akiwemo mkewe Faraja Kota.

Kama ambayo alitoa rai kwa wagombea wenzake jana wakati akitangaza nia, akiwataka waache kushambuliana na badala yake wadumishe umoja na kuwaheshimu viongozi waliotangulia, Nyalandu ameahidi kutokuwa “mlipa visasi.”

Akijibu swali kuhusu kudumisha Muungano, Nyalandu amesema ataudumisha muungano huo wa Taganyika na Zanzibar kwa sababu ni zaidi ya vyama vya siasa.

“Muungano wetu ni muungano wa mioyo, unazidi tofauti zetu za kidini, unazidi ukabila wetu na unazidi tofauti zetu za vyama vya siasa.

“Bila kujali nani atashinda, nitahakikisha ninashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha unadumu hadi nchi nyingine zije zijifunze maana ya utanzania wetu,”amesema.

Nyalandu ameongeza kuwa, iwapo atashinda nafasi hiyo ataiongoza nchi bila kulipa visasi kwa kuwa anaamini katika umoja wa kitaifa.

“Nataka kuona Watanzania wote tunafanya kazi kwa pamoja, naamini tukifanya hivyo tunaweza kuishangaza dunia,”alisema.

Alisema yeye anachukua fomu ya kuwania urais huku akizifahamu changamoto za Watanzania pamoja na kazi kubwa waliyoifanya marais wa waliotangulia.

“Nitahakikisha wazee wetu wanatunzwa vizuri, ikiwemo wazee wote waliowahi kuiongoza nchi yetu. Nitahakikisha tunawaendeleza vijana na wanawake, nitahakikisha vijana hawajioni mizigo katika nchi yao bali watapatiwa fursa ambayo itaishangaza dunia,”alisema Nyalandu.

NYALALI

Majira ya saa 7:00 mchana, ilikuwa zamu ya Peter Nyalali, ambaye alifika makao makuu na kukabidhiwa fomu yake ya kuomba kuteuliwa na CCM.

Nyalali ambaye si maarufu katika medani za kisiasa kama ilivyokuwa kwa baba yake mzazi, Jaji Nyalali, naye alipata muda wa kuzungumza na waandishi wa habari, akisema kugombea nafasi hiyo ni haki yake kikatiba, anataka kukuza demokrasia pamoja na kuleta mabadiliko chanya katika nyanja mbalimbali.

Amesema alikuwa afisa mwandamizi katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) hadi mwaka 2007, alipomuomba Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama atoke nje ya jeshi ili alitumikie Taifa katika nafasi nyingine.

“Mwaka 2010, niligombea ubunge Temeke, nikashika nafasi ya tatu. Mwaka huohuo nikagombea uspika lakini chama kikaona nipishe nafasi hiyo kwa kuwa ilikuwa zamu ya mwanamke,”amesema.

Alipoulizwa sababu za kuamua kugombea nafasi ya juu zaidi, Nyalali amesema alipogombea ubunge alipata kujua mahitaji ya Watanzania ni nini.

Akijibu kwa nini hakutangaza nia mapema kabla ya kuchukua fomu ili afahamike kama walivyofanya makada wenzao, Nyalali amesema siasa ni sayansi na kwamba siyo wote wanaomchagua rais.

“Watanzania wengi wananifahamu, nina kundi kubwa na nianaomba vyombo vya habari vinitangaze,”amesema.

Tofauti na wagombea wengine wanaoongozana na makundi ya watu na msafara wa magari, Nyalali alifika makao makuu ya CCM kuchukua fomu yake, akitumia usafiri wa gari ndogo ya kukodi (taksi).

MULENDA

Leonce Mulenda, ujio wake wa kuchukua fomu ulikuwa wa kushtukiza. Hakutangaza nia wala kuweka taarifa zake wazi mapema kwani hata kwenye ratiba ya leo jina lake halikuwemo,bali lilingizwa baadaye.

Amefika mchana wa saa nane, na kukabidhiwa fomu yake kasha akazungumza kwa kifupi akisema, iwapo atapata nafasi hiyo atahakikisha CCM inakuwa imara.

“CCM haitakuwa joka la mdimu, tutahakiksha Serikali inatekeleza ilani yake na watumishi wa umma wakati wote wataongozwa na sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa,”alisema.

Mulenda ameongeza kuwa, kinyume na hilo mtumishi huyo atakuwa anajichimbia kaburi lake.

Amesema, serikali yake kupitia ilani ya CCM, itakuwa ni sikivu, makini na inayojali shida za watu huku akijinasibu kuendeleza elimu.

error: Content is protected !!