January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nyalandu: Nassari hanibabaishi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (kushoto) akibadilishana mawazo na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasali

Spread the love

SIKU moja baada ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), kudai kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kazi yake ni kuzunguka maporini na kupiga picha, amejibu akisema kali hiyo haimbabaishi. Anaandika Mwandishi Wetu (endelea).

Amesema “mbunge kusimama bungeni na kutoa kashfa badala ya kueleza masuala ya kisera au kiutendaji ni kupungukiwa busara na jamii, hivyo hana budi kupuuzwa.

Akichangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni jana, Nassari alisema Nyalandu kazi yake kubwa ni kuzunguka katika mapori ya akiba na kupiga picha na askari pamoja na kushangaa mbwa wa kizungu na kupokea ndege na helikopta za msaada.

Alisema utendaji huo na mawaziri wengine unaweza ukawa ni ishara ya serikali iliyochoka.
Hata hivyo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Nyalandu amesema Nassari anapaswa kuwakilisha na kutetea wapigakura wake kwa hoja badala ya kuropoka masuala ambayo hayana tija.

“Kauli zinazotolewa na wapinzani bungeni akiwemo Nassari kuishutumu serikali kuwa imechoka na kujaribu kuichonganisha na wananchi, kamwe hakuwezi kuikatisha tamaa kwa kuwa uzushi kwa upinzani ni jambo la kawaida,”amesema.

Kwa mujibu wa Nyalandu, mapema mwaka huu, alifanya ziara wilayani Arumeru likiwemo jimbo la Nassari kutatua mgogoro baina ya wananchi na hifadhi, ambapo mbunge huyo alimtia moyo na kumtaka kupuuza kauli za kukatisha tamaa zinazotolewa dhidi yake.

“Hizi kauli za Nassari ni za kitoto na haziwezi kuleta tija kwa wapigakura wake…asimame kuzungumzia utendaji na masuala ya kisera sio kashfa ambazo hazipo…Namshauri awatumikie wapiga kura wake.

“Nilifanya ziara jimboni kwake kutatua mgogoro na alinitia moyo kutokata tamaa na kauli za watu wanaonibeza na kunipongeza kwa utendaji kazi wangu,” alisema Nyalandu katika taarifa yake.

Ameongeza kuwa, “Nassari katika mkutano wa viongozi wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, ambao pia ulihudhuriwa na mbunge wa Siha, Aggrey Mwanry, alisema “aomba kukutia moyo kwani anayefanya kazi ya Mungu utapata nguvu. Nikisikia mtu bungeni anasema wewe ni waziri mzigo, mimi nitaruka juu na kumwangukia vibaya’.

Kwa mujibu wa Nyalandu, ziara hizo zimeleta mafanikio makubwa kwa wizara yake kumaliza migogoro ya ardhi mingi kwa muda mfupi katika mapori ya akiba na hifadhi za taifa zenye migogoro ya ardhi na wananchi.

error: Content is protected !!