January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nyalandu azuia uingizaji mifugo Loliondo

Mifugo ikichungwa

Spread the love

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amepiga marufuku mifugo kutoka nchi jirani kuingizwa kwenye eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro na kuonya kuwa, ardhi iliyopo ni kwa ajili ya wafugaji wa Tanzania. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).

Amesema mifugo ya Watanzania itaendelea kubaki kuchungwa ndani ya ardhi yake na ile ya nje ibaki kwenye ardhi ya nchi zao na kwamba, mifugo yote kutoka nje itakayokamatwa itataifishwa na fedha zake kutumika kujenga maabara na madawati kwenye shule za msingi na sekondari.

Ameziagiza mamlaka zinazohusika kuhakikisha zinasimamia kikamilifu wimbi la mifugo kutoka nchi jirani kuingizwa nchini na kuzitaka jamii za wafugaji kwenye maeneo hayo kutowasaidia wanaotoka nje ya nchi kuingiza mifugo.

Nyalandu alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Olosokwani, Loliondo wilayani Ngorongoro muda mfupi baada ya kukagua na kuzindua miradi ya visima virefu 37, iliyofadhiliwa na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Miradi hiyo inalenga kumaliza tatizo la maji kwa wananchi wa wilayani hiyo, ambapo pia imehusisha maeneo maalumu ya kunywea maji wanyama.

Amesema serikali inaendelea na mikakati mbalimbali kuhakikisha inamaliza kero za wafugaji, lakini kuna baadhi ya wananchi na watendaji wa vijiji na kata wamekuwa kikwazo kutokana na kuruhusu mifugo kutoka nje kuingizwa nchini kwa njia za panya.

Kwa mujibu wa Nyalandu, eneo la Loliondo limekuwa miongoni mwa maeneo yenye migogoro mikubwa ya ardhi na kusababisha wafugaji ambao ni wazawa kutokuwa na maeneo ya kutosha kwa malisho ya wanyama.

“Ni marufuku mifugo kutoka nchi jirani kuingizwa hapa Loliondo na maeneo mengine ambayo yamehifadhiwa kisheria…hatutaki migogoro kabisa na ndio sababu tumekuwa tukitumia muda mwingi kusaka ufumbuzi wake.

“Naomba ardhi hii ni kwa ajili ya wafugaji wetu sio kutoka nchi jirani, wageni wakae mbali na Loliondo na tukikukamata umeingiza mifugo humu tunaitaifisha na fedha zake tunatumia kutengeneza madawati na maabara,” alisema.

Nyalandu pia alizionya taasisi zisizo za kiserikali ambazo zimekuwa sehemu ya migogoro wilayani hapa kuacha kuwavuruga wananchi kwa maslahi yao binafsi.

Alisema tabia ya baadhi ya wanaharakati ambao wamejazana Loliondo kwa lengo la kuchochea migogoro na kuwavuruga wananchi kamwe haikubaliki na kuwataka wananchi kuwa makini.

“Matatizo ya Loliondo hayawezi kutatuliwa na wanaharakati na ngo’s zilizopo hapa, ziseme zimewafanyia nini wananchi wa Ngorongoro zaidi ya kuwaingiza kwenye migogoro kila kukicha maslahi ya wachache.

“Rais Kikwete alishasema wafugaji watafanya shughuli zao kwa amani na wakulima pia, tabia za kuwavuruga wananchi ili mpate misaada kwa maslahi yenu ni usaliti kwa watanzania wenzenu. Tunataka maendeleo kwa ustawi wa Loliondo sio migogoro,” alisema Nyalandu.

Naye Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini, amesema serikali yake itaendeleza juhudi zake katika kusaidia wananchi wa Ngorongoro kuondoka na matatizo mbalimbali.

Amesema kwa sasa wamejipanga kumaliza tatizo la maji na ndio sababu wametoa fedha nyingi kwa ajili ya kuchimba visima virefu na vya kisasa ili kumaliza tatizo hilo.

error: Content is protected !!