January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nyalandu amaliza mgogoro Karatu

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (mwenye suti nyeusi) akipokea maelezo kutoka kwa mhifazi mkuu wa Saadan

Spread the love

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ameendelea kuipatia ufumbuzi migogoro ya ardhi na mipaka baina ya wananchi na hifadhi za taifa na mapori ya akiba nchini. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).

Tayari Nyalandu amefanikiwa kumaliza migogoro ya mipaka baina ya wananchi wa Mbarali ambao walikuwa na mgogoro mzito ulidumu kwa zaidi ya miaka saba na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wananchi wa Bagamoyo na Hifaddhi ya Taifa ya Saadani na sasa amegeukia mgogoro wa Misitu wa Marah na wananchi wa Kata ya Buger wilayani Karatu.

Katika kuhakikisha mgogoro unamalizika, Nyalandu alifanya ziara wilayani Karatu na kuunda Kamati Maalumu itakayokuwa chini ya Mkuu wa Wilaya hiyo Omar Kwaang’.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo watakuwa ni Ofisa Usalama wilaya, maofisa wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na wawakilishi wa wananchi.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Bugher juzi, Nyalandu alisema kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuchunguza uhusiano mbaya baina ya wananchi na wahifadhi na kushauri njia sahihi itakayomaliza tatizo hilo.

Amesema kamati hiyo itafanya kazi zake kwa wiki mbili na ilianza kazi rasmi juzi hiyo hiyo mara baada ya kumaliza kuzungumza na wananchi.

Awali, wananchi wa kata hiyo walilalamikia vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na askari wa hifadhi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini kubwa pindi wanapoingiza mifugo kuchunga ndani ya msitu huo.

Akitoa malalamiko hayo mbele ya Nyalandu, Elian Mboyah, amesema askari wa msitu huo wamekuwa na kawaida ya kuwapiga pindi wanapowakuta ndani ya hifadhi na kudai kuwa wakati mwingine silaha za moto hutumika.

Amesema wana imani kubwa kuwa ujio wa Nyalandu kijijini hapo utakuwa suluhisho la mateso wanayoyapata na kuomba, wahanga wa mateso ya wahifadhi hao wakaangaliwa kwa jicho la huruma akiwa na maana ya kupatiwa huduma za kijamii.

“Tumekuona waziri Nyalandu tuna imani mgogoro huu utakuwa na sura mpya ya amani na mahusiano mapya…tumechoshwa kunyanyaswa na askari hawa. Tunaomba wahanga wa mateso wakiwemo watoto, wajane na wazee wakaangaliwa kwani ndugu zao waliojeruhiwa ndio walikuwa tegemeo,” amesema Mboyah.

Kwa upande wake, Nyalandu amesema amesikia kilio cha wananchi hao na ndio sababu amefika eneo hilo kwa lengo la kutafuta mwafaka na kwamba, wahifadhi ni watanzania waliojitolea kulinda rasilimali, hivyo wasionekane kuwa maadui.

Amesema kuna kila sababu kwa wananchi na wahifadhi kuwa na mahusiano mazuri yenye kujenga na kuonya tena ni marufuku wananchi kupigwa ama mifugo yao kuteswa na kuuawa na kwamba atakayekiuka agizo hilo, atachukulia hatua kali za kisheria.

Pia, Nyalandu alizulu kaburi na kuzungumza na familia ya mwanakijiji anayedaiwa kupoteza maisha kwa kupigwa na askari wa wanyamapori na kukabidhi ubani wa Sh. 3 milioni.

Katika kuimarisha ujirani mwema na mahusiano mazuri baina ya wananchi na wahifadhi, Nyalandu alitangaza kuipatia Kata hiyo Sh. 100 milioni kama mchango wa Mamlaka ya Hifadhi Tanzania (TANAPA) kusaidia ujenzi wa madarasa.

Pia, alitangaza kutoa Sh.60 milioni 60 ambazo zitatumika kutekeleza mradi wa soko kwa ajili ya kuwawezesha akina mama wajasiriamali kuuza bidhaa na kujiongezea kipato.

Awali, Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso (Chadema), amesema ujio wa Nyalandu utasaidia kumaliza mgogoro huo na kuwataka wananchi kuweka itikadi za vyama pembeni na kuungana kuhakikisha tatizo hilo linamalizika.

Katika ziara hiyo, Nyalandu alifuata na maofisa wa wizara, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Allan Kijazi, ambaye aliongozana na maofisa wake mbalimbali, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania, Herman Killario pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Karatu.

error: Content is protected !!