Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Nyalandu aitosa CCM, haridhishwi na serikali ya Magufuli
Habari za SiasaTangulizi

Nyalandu aitosa CCM, haridhishwi na serikali ya Magufuli

Spread the love

MBUNGE wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amejiuzulu nafasi hiyo na kujiondoa CCM kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa siasa nchini, anaandika Mwandishi Wetu.

Pia Nyalandu amejiuzuru nafasi ya ujumbe wa Halmashauri kuu ya chama cha Mapinduzi CCM pamoja na nafasi zote ndani ya chama cha mapinduzi kuanzia leo Oktoba 30 mwaka 2017.

Soma taarifa kamili ya Nyalandu kujivua uanachama wa CCM na ubunge.

NIMEAMUA kujiuzulu NAFASI yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama kuanzia leo, Oktoba 30, 2017.

HALIKADHALIKA, asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job Ndugai, Mb., barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya UBUNGE wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 hadi Sasa.

AIDHA, Nimechukua UAMZI huo kutokana na kutorishwa kwangu na mwenendo wa hali ya Kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa HAKI za Kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania wenzetu, na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya MIHIMILI ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru uliainishwa na kuwekwa bayana KIKATIBA.

https://youtu.be/TuUSExHaq0w

VILEVILE, Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge na mahakama ambayo ndio chimbuko la Uongozi Bora wa nchi, na kuonesha kwa uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na kwamba Serikali ni ya Watu kwajili ya Watu.

MIMI Naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM, nikiwa nimekitumikia kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM TAIFA, kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania Sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo awali. AIDHA, Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna Moja au nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa TAIFA MWALIMU Julius Kambarage Nyerere.

HIVYO BASI, kwa dhamira yangu, na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na haki ya KIKATIBA, natangaza KUKIHAMA Chama Cha Mapinduzi CCM leo hii, na nitaomba IKIWAPENDEZA wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, basi waniruhusu kuingia MALANGONI mwao, niwe mwanachama, ili kuungana na CHADEMA na watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa ki demokrasia na uhuru wa mawazo.

VILEVILE, nimemua kujiuzulu KITI Cha Ubunge, Jimbo la Singida Kaskazini kuruhusu kufanyika kwa UCHAGUZI mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua ITIKADI wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye changamoto lukuki nchini Tanzania. Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili kwamba, SOTE kama TAIFA tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi yetu. Ni maombi yangu kwa MUNGU kuwa Haki itamalaki Tanzania. Upendo, amani na mshikamano wa watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi za Kisiasa, na makabila yote nchini uimarike. Tushindane ki sera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama ndugu, na TAIFA lililo imara na nchi yenye ADILI.

Mungu Ibariki Tanzania.
Lazaro S. Nyalandu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!