SIKU mbili baada ya kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lazaro Nyalandu, amesema chama hicho tawala ni imara kuliko Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Nyalandu ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, amesema alipohamia Chadema, ndio alipojua kwamba CCM ni imara zaidi, hivyo hakuwa na budi kurejea.
“…lakini ni kweli, nilikwenda upinzani na baada ya kufika huko nikabaini CCM ni chama madhubutu na ndiyo maana nimeamua nimerejea,” amesema Nyalandu ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wakati wa Utawala wa Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete.
Nyalandu ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, tarehe 3 Mei 2021, katika mahojiano maalum na kipindi cha Clouds360 cha Clouds Televisheni.
Mwanasiasa huyo alikuwa akijibu swali la kilichomtoa CCM kwenda Chadema kisha kurejea CCM ni ‘tumbo lake?’ amesema, “ningeondoka Chadema na kwenda NCCR-Mageuzi au TLP hiyo ingekuwa kutangatanga.”

Alipoulizwa ataikumbuka kwa lipi Chadema? amesema “wanachadema wengi ni watu wazuri sana, wanashauku kubwa, ukitaka kujua uzuri ambao wanawazidi CCM, itisha tu mkutano, watakuja wengi sana, kutoka maeneo mbalimbali.
“Lakini CCM, kimejaaliwa mifumo, itifaki ya chama, kuchaguana na kupokezana vijiti,” amesema Nyalandu, aliyedumu Chadema kwa siku 1,278
Pia, amekumbushia alivyoshambuliwa mitandaoni, mara baada ya yeye kwenda kushiriki maziko Chato, mkoani Geita ya Hayati Rais John Pombe Magufuli.

Amesema, baadhi ya wana Chadema walimshambulia ikiwa ni tofauti na alivyokwenda kumtembelea Nairobi nchini Kenya, Tundu Lissu, Makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara, baada ya kushambuliwa.
“Nilipokwenda Chato kuzika, nilipata mashambulizi si kutoka CCM bali kutoka Chadema.”
“Lakini Lissu alipopata matatizo, nilikwenda kumwona, sikupata mashambulizi kutoka CCM au kiongozi yoyote, ndiyo maana nasema, kule wimbo hauimbiki,” amesema Nyalandu
Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana tarehe 7 Septemba 2017, katika makazi yake Area D, jijini Dodoma akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge.
Mwanasiasa huyo alijiunga na Chadema tarehe 30 Oktoba 2017, ambapo tarehe 30 Aprili 30, katika mkutano mkuu maalum wa CCM, mbele ya mwenyekiti wake mpya, Rais Samia Suluhu Hassan, alirejea ‘nyumbani.’
time is the best judge behind God