April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Nusura ATCL wamwingize mkenge Rais Magufuli

Spread the love

MAOFISA wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), walikuwa kwenye hekaheka za kukwapua fedha za umma kupitia kauli ya Rais John Magufuli aliyoitoa tarehe 11 Januari 2019. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Ni baada ya Rais Magufuli kuagiza ATCL ichukue ndege ya serikali na kuingiza kwenye biashara ya kubeba abiria jambo ambalo lilionekana kuwa fursa kwa maofisa hao kutaka ‘kupiga’ pesa kupitia agizo hilo.

Kiongozi huyo wa nchi alitoa maagizo hayo wakati akipokea ndege ya tano ya ATCL aina ya Air Bus 200 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa jijini Dar es Salaam.

Ufafanuzi wa namna fedha hizo zilivyotaka kupigwa, umetolewa leo tarehe 28 Machi 2019 na Rais Magufuli wakati akikabidhiwa ripoti ya utendaji ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amesema, watumishi hao wa ATCL walitaka kutumia gharama kubwa katika kufanikisha zoezi la ubadilishwaji rangi katika ndege hiyo sambamba na uchoraji wa picha ya Twiga.

Amesema, watumishi hao walipanga kazi hiyo ifanywe na kampuni ya nje, badala ya kutafuta kampuni za ndani ili kupunguza gharama.

Na kwamba, alipowauliza sababu za kutaka kutumia kampuni za ndani, walijibu kwamba, hapa nchini hakuna mtu atakayeweza kufanya hivyo.

Amesema, licha ya kutoa ushauri huo watumishi hao walikaidi na kutafuta kampuni ya nje ambayo gharama zake zilikuwa ni zaidi ya milioni 200.

“…Wakasema haya maneno na kumchora Twiga hayawezi kufanyika nchini,  hayupo mtu wa kufanya hivi. Zikatafutwa nchi tatu za nje sitaki kuzitaja.

“Nikasema, jamani hapana tafute wataalamu wetu wanaweza kuchora. Wakaa kimya, wakafikiri nimesahahu wakawa wametafuta nchi Fulani,” amesema na kuongeza;

“Nikanyamaza, baadaye Jumapili moja nikaambiwa ndege inaondoka kesho asubuhi, watakaoisindikiza ndege kufanyiwa hiyo shughuli, wamelipwa Dola  28,000 ambayo ni mil 60, advance payment 60 percent (malipo ya awali) na zishalipwa ambapo gharama ni kama mil 200,” amesema.

Akionesha kukerwa na rushwa Rais Magufuli amesema, mtu yoyote akikamatwa na vitendo vya rushwa afikishwe mahakamani.

 “Siku tatu nne zilizopita nilipigiwa na raia fulani kwamba, tunaombwa rushwa na viongozi wa CCM ya milioni 5. Akasema, lazima tuwape sababu hiyo ndiyo kula yao, nikasema kwa nini hamjaenda takukuru.

“Wakajibu, tunaogopa watatuchoma. Nikawaambia hao wa CCM uwashike tena wakiwa wamevaa nguo za kijani,” amesema Rais Magufuli na kwamba, baadaye walikamatwa.

error: Content is protected !!