February 28, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Nusu ya wanafunzi vyuo vikuu wakosa mikopo

Mkurugenzi wa Idara ya Haki na Wajibu wa Wanafunzi Tanzania, Abdul Nondo

Spread the love

WANAFUNZI wa elimu ya juu wamezidi kuikaba koo  Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu  (HESLB), na kuitaka iwapatie mikopo, anaandika Faki Sosi.

Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo  Vikuu Nchini (TSNP), wametoa kilio hicho ikiwa ni siku chache tangu Rais John Magufuli kutangaza kwamba hakuna mwanafunzi wa elimu ya juu atakayekosa mkopo.

Juni 2  mwaka 2016  Rais Magufuli alisema hayo alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo kuku cha Dar es Salaam (UDSM)  kampasi ya Mlimani.

Mkurugenzi wa Idara ya Haki na Wajibu wa Wanafunzi Tanzania,  Abdull Nondo ameomba serikali kuchukua hatua za dharura ili kuwapatia mikopo wanafunzi hao.

“Serikali ilichukulie suala hili kama dharua na kutoa mikopo kwa wanafunzi hawa wenye vigezo kama yalivyo mafuriko”

Nondo ameeleza kuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza  wametengewa fedha Sh. bilioni 108.8 ambapo HELSB imeeleza kuwa itatoa kwa wanafunzi 30,000  wakati waliomba wanafikia 61,000
Mmoja wa viongozi wa TSNP, Sity Ngwali ameeleza kuwa serikali inatakiwa kulipa kipaumbele suala hilo na kwamba  walitazame kwa jicho la tatu.

Wanafunzi hao walikusanyika leo katika ofisi za HESLB zilizoko Mwenge jijini Dar es Salaam hivyo kusababisha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kufika eneo hilo.

Baadhi ya wanafunzi waliangua vilio walipozungumzia shida  wanazopata kutokana na majina yao kutoonekana katika orodha ya wanaopata mikopo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa HESLB, Omega Ngole amesema jukumu lao ni kuwapokea na kusikiliza hoja za wanafunzi hao kabla ya kuzifanyia kazi.

Amesema wamewataka wanafunzi hao kuorodhesha majina ili waangalie ni wapi walikosea na kuwapa majibu au kufanyia kazi changamoto zao.

error: Content is protected !!