December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nusrat Hanje ashangaa Chadema kumteua mbunge kisha kumkataa hadharani

Mbunge wa Viti Maalum asiye na chama bungeni, Nusrat Hanje

Spread the love

 

MBUNGE Viti Maalum, Nusrat Hanje, amedai alikosa nafasi ya kujitetea kwa mdomo katika Baraza Kuu la Chadema, Ili kueleza viongozi wake waliomteua na kumkataa mbele za watu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Nusrat ametoa madai hayo leo Ijumaa, tarehe 4 Novemba 2022, katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, mbele ya Jaji Cyprian Mkeha, kwenye Kesi Na. 36/2022, iliyofunguliwa na wabunge viti maalum 19, wakiongozwa na Halima Mdee, kupinga kuvuliwa uanachama wa Chadema.

Ni wakati akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa Mjibu Maombi namba moja katika kesi hiyo (Bodi ya Wadhamini ya Chadema), Peter Kibatala, kuhusu malalamiko aliyowasilisha mahakamani hapo kupitia hati yake ya kiapo.

Nusrat alidai, mtu anapoitwa kwenye kikao inabidi asikikizwe kwa kile alichodai kurasa tano alizotumia kuandika hoja zake za kukata rufaa Baraza Kuu la Chadema, kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kumvua uanachama, hazikutosha kujitetea.

Alitoa madai hayo baada ya Wakili Kibatala kumhoji kama anafahamu kuna namna mbili za kusikilizwa, kwa mdomo na maandishi.

“Ukishaniita kwenye kikao inabidi unisikikize sababu kulikuwa na uwezo wa kuniita….ndio maana nikasema page (kurasa) tano hazikunitosha kueleza viongozi wangu walioniteua na kunikataa mbele za watu. Ukiniita lazima unisikilize,” amedai Nusrat.

Wakili wa Chadema, wakiongozwa na Peter Kibatala (katikati) wakiwa mahakamani

Baada ya Nusrat kutoa majibu hayo, Wakili Kibatala alimhoji kama katiba ya Chadema imeweka sharti kwa mtu anayekata rufaa kwenye Baraza hilo, kuwasilisha sababu zake kwa njia ya maandishi na mdomo.

Ambapo Hanje amedai hakumbuki kama kuna kifungu kinachozungumzia jambo hilo, “lakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaelekeza mtu kupewa nafasi ya kujitetea Ili kukidhi matakwa ya upatikanaji haki.”

Mdee na wenzake wamefungua kesi hiyo kuomba mahakama ifanye mapitio dhidi ya mchakato uliotumika kuwavua uanachama, wakidai haukuwa halali kwani hawakupewa nafasi ya kusikilizwa.

Nusrat ambaye aliteuliwa Mbunge Viti Maalum akiwa mahabusu akikabiliwa na kesi ya jinai Na. 115/2020, katika Mahakama ya Mkoa wa Singida, anaendelea kuhojiwa na Wakili Kibatala.

Mbunge huyo viti maalum, aliapishwa na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, tarehe 24 Novemba 2020, ikiwa ni muda mfupi tangu aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, kumfutia mashtaka yaliyokuwa yanamkabili.

Awali akihojiwa na Wakili Kibatala, Nusrat alidai alishindwa kuhudhuria mbele ya Kamati Kuu ya Chadema kujibu tuhuma zilizokuwa zinamkabili, kwa kuwa alichelewa kupata barua ya wito na kuomba angozewe muda wa kuandaa utetezi wake kwani alikuwa anashughulikia masuala ya kifamilia baada ya kutoka jela tarehe 23 Novemba 2020.

error: Content is protected !!