January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ntunzwe amuangukia Rais Samia kutekeleza agizo la Rais Magufuli

Spread the love

 

Mfanyabiashara Ramadhan Hamis Ntunzwe wa Dar es Salaam amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kumsaidia kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kumlipa fidia baada ya TRA kumsababishia hasara ya zaidi ya Sh milioni 800. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Hatua hiyo imekuja baada ya kupita miaka miwili na ushee tangu Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli alipoingilia kati sakata hilo na kuagiza Mamlaka hiyo kumlipa fidia hiyo.

Licha ya kwamba Rais Magufuli alitoa agizo hilo tarehe 7 Juni 2019, pamoja na vikao mbalimbali vilivyofanyika kabla ya Rais Magufuli kufariki tarehe 17 Machi, 2021, hadi sasa hakuna fedha yoyote aliyolipwa.

Sakata la Ntunzwe linaanzia 2017 alipokuwa akisafirisha mzigo wake kutoka Zambia kupitia mpaka wa Tunduma. Baada ya kufika Mbezi, Dar es Salaam, alikamatwa na maofisa wa TRA waliomdai rushwa ya Sh milioni mbili lakini alikataa kuwapa fedha hizo.

Baadaye suala hilo lilichukua sura mpya baada ya maofisa hao wa TRA kumbambikia makosa ya kukwepa kodi na hatimaye kutaifisha mali zake, huku nyingine zikiharibiwa na kuporwa fedha taslimu kiasi cha Sh milioni 60.

Ntunzwe anadai kuwa hasara ya kutaifishwa na kuharibiwa mali zake katika jaribio la mali hizo kupigwa mnada na kuibiwa kwa fedha taslimu, vilimsababishia hasara inayofikia Sh milioni 821.

Aidha, akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 11 Januari, 2022 jijini Dar es Salaam, Mfanyabiashara Ramadhan Hamis Ntunzwe baada ya agizo hilo la Rais Magufuli wakati huo, tarehe 26 Novemba, 2020 alipigiwa simu na ofisa kutoka wizara ya fedha na mipango kufahamishwa kuhusu taarifa  ya kikao kati yake na Kaimu Katibu mkuu wa wizara hiyo.

Amesema kikao hicho cha kwanza kilichohusisha maofisa kutoka wizara ya fedha na TRA, kilifanyika tarehe 2 Disemba 2020, ambapo Katibu mkuu huyo alimueleza kuwa kutafanyika vikao vitatu pekee kisha atalipwa pesa yake.

Amesema katika maelezo ya katibu mkuu huyo, alimhoji iwapo ameishtaki TRA mahakamani au lah, lakini alijibu kuwa hajawahi kuishtaki TRA bali mamlaka hiyo pamoja na kampuni moja ya udalali ndio iliyomshtaki lakini katika kesi hiyo aliwashinda.

Mfanyabiashara huyo ameendelea kutiririka kuwa, baada ya kutoa majibu hayo kikaoni, mwanasheria wa TRA aliyehudhuria kikao hicho alishikilia msimamo kuwa mfanyabiashara huyo ndiye aliyewashtaki na wala si TRA iliyomshtaki.

Amesema kutokana na mabiashano hayo kikao hicho kiliahihirishwa hadi tarehe 15 Februari 2021 ambapo aliwasilisha hati ya hukumu ya kesi hiyo aliyokuwa ameshtakiwa na TRA kisha mwanasheria huyo wa mamlaka hiyo akakiri katika kikao cha kwanza alikuwa ameghafirika.

Amesema baada ya maelezo hayo kikao hicho kilifikia maamuzi ya kuahirisha kikao hicho cha pili ambacho kilifanyika jijini Dar es Salaam ambapo katibu mkuu huyo wa wizara ya fedha aliahidi katika kikao cha tatu ambacho kitafanyikas Dodoma ndipo maamuzi ya kulipwa pesa yake yatafikiwa.

Amesema kwa bahati mbaya, msiba wa kitaifa uliotokea tarehe 17 Machi ulisababisha kikao hicho cha tatu kutofanyika.

Amesema alisubiri hadi  Juni mwaka jana ambapo aliandikia barua wizara ya fedha kukumbushia ahadi ya malipo yake katika kikao cha tatu lakini hakujibiwa.

Amesema hata alipoandika barua nyingine Agosti kwenda kwa waziri mkuu na Rais bado hakujibiwa.

“Kutokana na hali hiyo, namuomba Rais Samia kwa kuwa ni mtu wa Mungu asiyependa kuona wananchi wake wakidhulumiwa, namuomba sana anisaidie nilipiwe haki yangu. Hiio ni fidia ambayo nimepoteza fedha nyingi,” amesema.

Amesema licha ya madhila yote hayo, bado amekuwa akiandamwa na matapeli ambao wamekuwa wakimdanganya kuwa wametumwa na viongozi mbalimbali wa serikali jambo ambalo si kweli.

error: Content is protected !!