October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nondo: Maumivu ya Chadema tunayahisi ACT–Wazalendo 

Spread the love

CHAMA cha ACT – Wazalendo kitaendelea kupigania umoja na mshikamano ndani na nje ya chama kwa lengo la kuunga mkono mikakati ya kuirudisha nchi kwenye utawala wa sheria. Anaripoti Jabir Idrissa, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 12 Machi 2020 na Abdul Nondo, Mwenyekiti mpya wa Ngome ya Vijana wa ACT – Wazalendo alipokuwa akikabidhi Sh. 400,000 taslim kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili kusaidia kupatikana fedha za kuwezesha kuwalipia viongozi wa juu wa Chadema waliohukumiwa faini ya zaidi ya Sh. milioni 350 au kutumikia kifungo cha miezi mitano gerezani kutokana na kesi ya tuhuma za uchochezi ya mwaka 2018.

Nondo amesema vijana wa ACT – Wazalendo wamehamasika kuchangia fedha kufuata msimamo wa kiongozi mkuu wao, Zitto Zuberi Kabwe, aliyesema magumu wanayopitia viongozi wa Chadema yanawahusu pia wao kwa k uwa wamo katika harakati za kusimamisha demokrasia kamili nchini.

Kwa kuanzia, vijana wa ACT – Wazalendo wamechangia kiasi hicho na kuamua kukikabidhi haraka hatua ya kuthibitisha walivyoguswa na maumivu ambayo vijana wenzao wa Chadema wanapata kutokana na viongozi wao wanane kukutwa na hatia katika kesi ya tuhuma za uchochezi waliyofunguliwa Februari 2018.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam chini ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba ilitoa hukumu hiyo tarehe 10 Machi 2020, kwa viongozi wa Chadema akiwemo Freeman Mbowe, mwenyekiti wao, na wajumbe kadhaa wa Kamati Kuu. Taratibu za kulipia  faini zinaendelea huku wahukumiwa wakiwa gerezani.

Nondo amesema ACT – Wazalendo kinaamini mikakati ya kuirudisha nchi kwenye demokrasia na utawala wa sheria inahusu kila kijana wa Tanzania pasina kujali yu mwanachama au laa. “Kila kijana Mtanzania anapaswa kuyahisi maumivu wanayopitia viongozi wa Chadema kwani wanapigania demokrasia na maendeleo ambayo ndiyo mahitaji halisi ya vijana wote nchini… tutaendelea kuchangia huku tukihamasisha vijana wenzetu kote nchini kutuunga mkono,” amesema Nondo aliyefika makao makuu ya Chadema, Kinondoni Dar es Salaam akiandamana na ujumbe mzito wa wasaidizi wake.

Wasaidizi hao ni Abeid Khamis Bakar, Katibu wa Ngome anayesubiri kuthibitishwa na Halmashauri Kuu ya ACT – Wazalendo, Melista Joseph, Katibu wa Ngome Mkoa wa Dar es Salaam na Kijana Wambura, Katibu wa Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye hafla hiyo akiwakilisha uongozi wa Chadema, Hemed Ali, Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani inayohusisha mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, amesema kipindi kigumu wanachopitia viongozi wa Chadema pamoja na vyama rafiki kama ACT – Wazalendo ni ishara ya mtihani mkubwa wa ukandamizaji haki za raia unaokabili taifa.

“Hii changamoto wanayopitia viongozi wetu inawahusu wote nchini, wala haizingatii itikadi ambayo mtu anaamini. Tunaona wanaoumia chini ya utawala wa miaka minne sasa si wanasiasa pekee, wamo wafanyabiashara wanaoshtakiwa kwa kesi za (utakatishaji  fedha) na watu wengine kadhalika,” amesema.

error: Content is protected !!