December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

NMB yazindua mfumo wa majaribio ya kitekinolojia, BoT yapongeza

Spread the love

 

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imezitaka taasisi za kibenki nchini, kuanzisha au kubuni masuluhisho mbalimbali yanayowakabili wananchi ikiwemo ukosefu wa ajira na njia bora ya kuchochea maendeleo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, tarehe 21 Oktoba 2021, jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa BoT, Dk. Bernard Kibesse wakati akizindua Mfumo wa Majaribio ya Kitekinolojia wa Benki ya NMB (NMB TechHub).

Mfumo huo utawawezesha watu binafsi, kampuni au taasisi za kifedha kwenda na wazo la suluhisho lao kulifanyia kazi katika NMB TechHub, endapo wazo lao likipita litapelekwa BoT ambao nao wataliangalia kama lina tija na wakilipitisha, litatangazwa na kuanza kufanya kazi.

Mshindi wa wazo lake, litaingizwa kwa jamii akitumia mifumo ya NMB nchi nzima. Wazo linaweza kuwa la kutuma na kupokea fedha, kuangalia salio, kununua bidhaa mbalimbali na mengine mengi.

Dk. Kibesse amesema, kuna wabunifu wengi nchini ambao wanashindwa kufikia fursa ya kutekeleza yale waliyobuni na kuyangundua kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha “sasa wamepata sehemu ya kufanyia maboresho haya.”

“BoT inatambua changamoto mbalimbali zinazokutana nazo wananchi wanapohitaji kupata huduma za kibenki kama umbali na gharama, sasa kupitia NMB, imewawekea eneo la kwenda kuonesha, sasa kazi kwao,” amesema.

Dk. Kibesse amesema “huu ni wakati sasa kwa kampuni changa na watu binafsi kutengeneza suluhisho ili kupunguza gharama za kibenki kwa watu wote na ajira kwa vijana wetu. Naishukuru sana NMB kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kutatua changamoto mbalimbali.”

Aidha, Naibu Gavana huyo ameishukuru benki hiyo kwa kutenga Sh.100 bilioni kwa ajili ya kukopesha wananchi kwenye sekta ya kilimo kwa riba ya chini ya asilimia 10 na kuwa benki ya kwanza kutoa mikopo kwa riba hiyo.

Amesema, Benki Kuu ya Tanzania imekwisha kutenga fedha kwa ajili ya kuzikopesha benki ili kuchochea sekta za kibenki kukopesha wananchi na kutoza riba chini ya asilimia kumi.

“BoT iko tayari kuyapa mabenki mikopo kwa chini ya asilimia tatu na ninyi muende sasa kuangalia mtafanyaje. Kama umepata kwa asilimia tatu, sasa si unaweza kuamua ukawapa kwa asilimia nane, ubunifu ukaendelea na BoT tuko tayari kuwasaidia,” amesema

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alisema, baada ya kutambua umuhimu wa kampuni hizi za ubunifu, “tumeona tuzindue mfumo wa majaribio wa masuluhisho mbalimbali ambao utaruhusu watu na kampuni mbalimbali kuja kufanya majaribio ya mfumo huu.”

“NMB tunarahisisha huduma za kibenki kwa wateja wetu na Watanzania kwa ujumla, kwa sababu teknolojia ndiyo njia rahisi kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi kwa kutumia gharama nafuu,” amesema Zaipuna.

Kuhusu ubora wa mfumo huo wa ‘Sandbox Environment,’ Ruth amesema “utaendelea kulinda taarifa zetu za benki, tutawaruhusu kuja kufanya na kutumia taarifa mbalimbali tulizonazo. Kutakuwa na usiri mkubwa sana hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi kabisa.”

“Vijana wetu au Watanzania, sasa watapata sehemu mwafaka wa kufanya majaribio yao na kama watafanikiwa kwa suluhisho lao, watashirikiana na NMB kuzindua na kulitambulisha kwa wananchi ili lianze kutumika,” amesema

Mtendaji mkuu huyo amesema, wametenga fungu maalum la Sh.1 bilioni, itakayotumika kama mtaji, kuyaingiza hayo masuluhisho au bidhaa sokoni “kwani vijana wengi wanashindwa kufikia ndoto kwa kukosa mitaji.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Dk. Edwin Mhede amesema “NMB imeamua kufanya jambo hili kama sehemu ya benki na utekelezaji wa sera za umma. Teknolojia unapoanza ni ‘high risk’ kwani unapoanza kufanya jambo kuna uwezekano wa kushindwa.”

“Sasa ni wakati kwa vijana, kampuni na watu binafsi kutumia hii fursa kwa uaminifu. NMB imeamua kufanya hivyo si kuwasaidie ninyi bali jamii kwa ujumla. Sisi ni watu wa viwango. Usiri wa taarifa za wateja na miamala utakuwepo mkubwa na hautaathiriwa kwa vyovyote vile,” alisema

Naye Afisa Mkuu Teknolojia na Mabadiliko ya Digitali, Kwame Makundi amesema imewachukua miaka mitatu kuja na kitu kama hicho cha kuwaweka pamoja wabunfu kuja na suluhu za kidigitali kwenye sekta ya kibenki.

“Kwa sasa tumepata njia sahihi ya kuwasaidia wabunifu kwa kuwa sekta ya kibenki inakua kwa kasi, tunahitaji huduma nyingi ikiwemo za bima, miamala na uwekezaji kuwa katika mifumo ya kidijitali,” amesema Makundi.

error: Content is protected !!