October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

NMB yawatengea bilioni 100 wakulima, wafugaji na wavuvi

Spread the love

 

BENKI ya NMB nchini Tanzania imetangaza fursa kwa wadau wa kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuwatengea zaidi ya Sh.100 bilioni za mikopo yenye riba nafuu ili kuendeleza shughuli zao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi tarehe 7 Oktoba 2021, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema, mikopo hiyo ya riba nafuu itaanza kutolewa tarehe 15 Oktoba mwaka huu katika matawi ya benki hiyo nchi nzima.

“Mikopo hiyo itatolewa kwa kiwango cha riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka,” amesema Ruth. 

Amesema, wanufaika wa mikopo hiyo ni “wakulima, wauzaji wa pembejeo, watoa huduma, wajasiriamali na wasindikaji wadogo na wa kati wanaojishughulisha na shughuli zote katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi.”  

Mifugo ya Ng’ombe

Afisa mtendaji mkuu huyo amesema, hatua hiyo inalenga kupanua wigo wa wadau wengi katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi kupata mikopo yenye riba nafuu ambayo itaongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi. 

“Mteja ataweza kuwa na unafuu wa gharama ya mkopo na hivyo kuweza kujitengenezea faida zaidi. Faida hiyo inaweza kutumika kuongeza uzalishaji wa chakula, malighafi za viwanda na kuchagiza maendeleo ya viwanda nchini,” amesema Ruth. 

Akijibu masharti ya wanufaika, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki hiyo, Filbert Mponzi amesema masharti yatakuwa yaleyale kama ambayo wamekuwa wakiyatumia kwenye kituo mikopo kwa wajasiriamali.

Wavuvi wakiwa kazini

Mponzi amesema, wahitaji wakifika katika matawi ya benki hiyo 225 yaliyopo maeneo mbalimbali nchini, watapata masharti na kutakuwa na uwezo wa mtu mmoja, kampuni, vyama vya ushirika kukopa kuanzia kiwango cha chini Sh.200,000 hadi Sh.1 bilioni.  

“Mkopaji huyu anaweza kuwa mtu binafsi, chama cha ushirika, kampuni au taasisi yeyote itakayokidhi masharti ya ukopeshaji,” amesema Mponzi

Katika hatua nyingine, Ruth akizungumzia suala la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutenga fedha zaidi ya Sh.1  trilioni kwa ajili ya wakulima, amesema mpango wa NMB kuja na utaratibu huo ni wao hauhusiani na utaratibu wa BoT, lakini wataangalia namna ya kuongezea kwenye utaratibu walio nao. 

“Hili ni la kwetu NMB, tukiwa na lengo la kuwasaidia wananchi, lakini fursa iliyotangazwa na BoT tutaitumia pia kwa ajili ya kuwanufaisha zaidi wateja wetu. Hii Sh.100 bilioni tuliyoiweka haina muda maalumu, ikiisha tutafanya tathmini ikiwezekana tutaiongeza,” amesema.

error: Content is protected !!