July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NMB yavutia wabunifu suluhisho za kifedha, Dk. Mpango agusia vijana

Spread the love

 

MFUMO wa majaribio wa suluhishi za kifedha ulioandaliwa na Benki ya NMB umefungua wigo wa kuwawezesha wabunifu kujaribu suluhisho zao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Tayari wabunifu 150 wamevutiwa na wanaendelea kujaribu suluhishi zao na hii ni kwa kipindi cha miezi sita tangu kuzinduliwa.

Hayo yameelezwa jana Alhamisi, tarehe 19 Mei 2022 na Mkuu wa Idara ya Ubunifu wa Benki ya NMB, Josina Njambi alipokuwa akimueleza Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango alipotembelea banda la NMB katika hafla ya kufunga Wiki ya Maonesho ya Kitaifa ya Ubunifu Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Josina alimueleza Makamu wa Rais katika kuonesha namna benki hiyo inathamini wabunifu, walitengeneza mfumo maalumu ujulikanao kama NMB Sandbox environment ambao unatoa fursa kwa wabunifu wa suluhishi za kifedha hasa za kidigitali kujaribu suluhishi zao na kwa zitakazo fuzu kupewa fursa ya kushirikiana na Benki ya NMB katika kuzitekeleza.

“Mfumo huu unatoa fursa kwa wabunifu kuzijaribu suluhisho walizobuni na kuona namna zinavyoweza kufanya kazi kwa ufasaha na kwa ambao watafuzu katika majaribio haya watapata fursa ya kushirikiana na Benki ya NMB kwaajili ya kuziendeleza na kuzioanisha moja kwa moja na mifumo ya benki na kuanza kutumika katika utoaji wa huduma za kifedha kwa urahisi, usalama na haraka,” alisema Josina.

“Mbali na kutoa fursa zitakazo wanufaisha wabunifu hawa, masuluhisho bora ambayo yatafuzu yatakuwa chachu ya maendeleo makubwa katika sekta ya fedha hapa nchini na uchumi wa Taifa kwa ujumla.”

“Tunafurahia kuona wabunifu wamekuwa na muitikio mkubwa katika hili na tayari wabunifu 150 wameshajisajili katika mfumo huu na suluhisho zao zinaendela katika majaribio, tunaamini idadi hii itaendelea kuwa kubwa kwani bado fursa hii ipo kwa wabunifu na tutumie nafasi hii kuendeleza kuwakaribisha wabunifu wa suluhisho za kifedha kuja katika hii sandbox environment na kuzijaribu suluhisho walizobuni,” aliongeza Josina.

Aidha, Makamu wa Rais, Dk. Mpango alionesha kuvutiwa na jambo hilo la Benki ya NMB kuwajali na kutengeneza fursa za majaribio kwa wabunifu na kuwasisitiza kuwajali Zaidi Vijana wa Kitanzania wanaoleta ubunifu wao katika huo mfumo uliotengenezwa.

“Hongereni sana na niwaombe mzidi kuwajali zaidi Vijana wa kitanzania wanaokuja na masuluhisho hayo ya Kifedha,” alisema Dk. Mpango

Kwa upande wake, Katibu mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Eliamani Sedoyeka aliendelea kuwapongeza NMB kwa kuwajali wabunifu lakini pia kuwasihi kuendeleza ushirikiano mwema na wizara ya Elimu kwa maslahi mapana ya Elimu na ustawi wa Taifa kwa ujumla.

error: Content is protected !!