November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

NMB yatwaa tuzo ya MasterCard

Spread the love

 

BENKI ya NMB imekuwa benki ya kwanza nchini kupata tuzo ya MasterCard kutokana na mafanikio makubwa waliyoyaonesha kwa wateja wao katika matumizi ya kadi wakati wa kufanya miamala ya kibenki badala ya kutumia fedha taslimu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tuzo hiyo imekabidhiwa mwishoni mwa wiki na Meneja wa MasterCard Afrika Mashariki, Shehryar Ali kwa uongozi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam.

Ali alisema dunia kwa sasa ipo katika mikakati ya kupunguza matumizi ya fedha taslimu kwa kuwa zina gharama kubwa katika kuzitengeneza, kuzisafirisha lakini pia ni hatari kuwa nazo kiusalama.

“Tuzo hii ina maana kubwa kwa Benki ya NMB kama benki ya kwanza Tanzania kuwa na watumiaji wengi wa MasterCard, ninatoa pongezi kwa maono ya Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna pamoja na timu nzima ya NMB kwa kazi kubwa mnayoifanya kubadili mfumo wa miamala kuwa kidijitali,” alisema Ali.

Alisema haiangaliwi tu huduma au bidhaa inayotolewa na benki hiyo bali ni watu wangapi inawafikia tena kwa ufanisi mkubwa, hilo ndilo lililowasukuma kuwapa tuzo hiyo kama ishara ya kutambua ubunifu a kazi kubwa wanayoifanya kuiamsha jamii kupunguza matumizi ya fedha taslimu.

Naye Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi alisema ni heshima kwao kutambulika kimataifa kuwa benki inayokuza matumizi ya kadi kwa kiasi kikubwa kwenye kufanya miamala.

“Tuzo hii ni kielelezo tosha kabisa cha ukubwa wa benki ya NMB nchini inayochagizwa na upana wa mtandao wake wa matawi 226 na wateja zaidi ya milioni nne.”

“Hii ni tuzo ya kwanza ya namna hii kuwahi kutolewa kwa benki hapa nchini Tanzania. Asanteni sana wenzetu wa Mastercard na pia shukrani nyingi kwa wateja wa NMB waliotufanya kutambuliwa na Mastercard,” alisema Mponzi.

Alisema wamepata tuzo hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo idadi kubwa zaidi ya wateja wanaotumia kadi kuliko benki yoyote nchini.

“Zaidi ya wateja wa NMB milioni tatu wanatumia kadi za Mastercard kwaajili ya huduma mbalimbali za kifedha na hii ni idadi kubwa zaidi kufikiwa na benki yeyote nchini,” alisema

Mponzi alisema, beki hiyo itaendelea kubuni suluhisho mbalimbali zenye lengo la kuboresha matumizi ya kadi na kwa kutumia teknolojia mbalimbali, huduma hizi zitazidi kuwa bora zaidi. Ni imani yetu kuwa idadi ya watumiaji wa kadi itazidi kuongezeka na hata miamala kupitia kadi itaongezeka zaidi.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Biashara ya Kadi, Benki ya NMB, Philbert Casmir alisema kwa muda mrefu sasa benki hiyo imejikita katika ubunifu, mfumo wa kidijitali na mambo mengine yanayowaletea unafuu wateja wao wakati wa kupata huduma.

Alisema mwaka huu, beki hiyo imekuwa ikipata tuzo mbalimbali za kimataifa zaidi ya sita, ambazo kwa kiasi kikubwa inajipambanua kuwa karibu na wateja wake, hivyo wameahidi kuendelea kubuni suluhisho mbalimbali zenye lengo la kuboresha matumizi ya kadi na kwa kutumia teknolojia mbalimbali.

error: Content is protected !!