BENKI ya NMB imekabidhi vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh90 milioni kwa Timu ya Bunge huku wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Vifaa vilivyokabidhiwa ni fulana, traksuti na vifaa vingine vya michezo ikiwa ni pamoja na kutoa kifungua kinywa kwa wabunge wote na wageni pamoja na kuwawekea mahema yatakayotumika katika bonanza hilo ambapo ufadhili huo kwa ujumla wake unagharimu Sh130 milioni.

Vifaa hivyo ni kwa ajili ya bonanza la michezo mbalimbali itakayofanyika kesho Jumamosi, Septemba 2,2023 jijini Dodoma na kuongozwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zuber, Ali Maulid.
Akikabidhi vifaa hivyo leo Ijumaa, Septemba 1, 2023 kwa Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Festo Sanga, Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango amesema wanatoa vifaa hivyo katika muendelezo na utaratibu wao kwa taasisi za Serikali na wadau wengine kwani ndiyo utaratibu waliojiwekea.
Shango amesema utoaji wa vifaa hivyo siyo mara ya kwanza na haitakuwa mwisho kwani wanaendelea kuamini kuwa Taifa bora ni lile linalojali afya za watu wake ikiwemo kwenye michezo.
Meneja huyo wa kanda ya kati amewaomba wabunge kuendeleza ushirikiano na benki hiyo kwa kuwa ni wadau ambao wanapaswa kufanya shughuli zao kwa pamoja kwani wote wanawahudumia wananchi.
“Lakini tuwaombe wabunge na wananchi kuendelea kuitumia benki yenu ya NMB kama ambavyo tumeendelea kuwa wamoja na sisi tunaahidi pamoja nanyi kwa kila jambo ili mradi tujenge nchi yetu kwa kuwa na watu wenye afya njema,” amesema Shango.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Mwenyekiti wa Bonanza la Bunge, Fessto Sanga amesema msaada huo kutoka NMB siyo mara ya kwanza na kwa mwaka huu imekuwa ni mara ya pili wakiwafadhili.
Amesema katika bonanza la kwanza walipokea vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh100 milioni jambo linalofanya kwa mwaka huu pekee wamepata ufadhili wa zaidi ya Sh230 milioni kutoka benki hiyo.
Sanga amesema vifaa vilivyotolewa na NMB vinawasaidia kwenye mabonanza yao ikiwemo michezo itakayofanyika kesho Jumamosi, tarehe 2 Septemba 2023 ambalo ni maalumu kwa mashindano ya wabunge na watumishi wa ofisi ya bunge.
Kwa upande wa wabunge watashirikiana na wenzao wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na michezo itaanzia Chuo cha Mipango Dodoma kuelekea Viwanja vya Jonmerini.
Mbunge huyo wa Makete amesema mgeni rasmi katika bonaza hilo lenye lengo la kupambana na magonjwa yasiyo na kuambukiza atakuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Zuber, Ali Maulid.
Mwenyekiti huyo ametaja michezo itakayokuwepo katika bonanza hilo ni Mpira wa miguu, pete,bao, kukimbia, mwendokasi, kupita kwenye pipa na mingine.
Leave a comment